1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande zinazohasimiana Libya zatoa wito wa kusitisha mapigano

Saleh Mwanamilongo
21 Agosti 2020

Pande zote mbili katika mgogoro wa Libya zimetoa mwito wa kusitisha mapigano nchini humo na kutangaza kuitishwa kwa uchaguzi mkuu ifikapo Machi mwakani. Hatua hiyo imepongezwa na Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/3hJ6q
Libyen Minsterpräsident Fayiz as-Sarradsch
Picha: AFP

Waziri Mkuu wa serikali ya Tripoli inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, Fayez al-Sarraj, ametangaza siku ya Ijumaa usitishwaji mapigano kote nchini Libya. Sarraj ametoa pia wito wa kuondoa wapiganaji katika wamji Sirte ambao unadhibitiwa na vikosi vya upinzani. Kwenye taarifa tofauti, Aguila Saleh, spika wa bunge lenye makao yake mjini Sirte alitoa mwito wa kusitishwa mapigano.

Taarifa hizi zimetolewa wakati kulikuweko na hofu ya kuzuka upya kwa mapigano katika nchi hiyo ambayo imekumbwa na ghasia kwa miaka tisa sasa. Waziri mkuu wa serikali ya umoja wa kitaifa ya mjini Tripoli, Fayez Sarraj alitangaza pia kwamba uchaguzi wa rais na bunge utaitishwa mwezi Machi mwakani.

Vizuizi viondolewe

Pande zote mbili zimetaka kuondolewa kwa vizuizi katika sekta ya mafuta, vilivyowekwa mapema mwaka huu na kamanda wa vikosi vya mashariki mwa Libya, Khalifa Haftar. Haftar ni mshirika wa spika wa bunge la mashariki, Aguila Saleh.

Pande hizo hasimu zilitoa pia mwito wa kurejeshwa kwa ushuru wa mafuta na kuelekezwa kwenye akaunti ya benki ilioko nje ya nchi  ya kampuni ya kitaifa ya mafuta. Mwanzoni mwa mwaka huu, viongozi wa makabila yenye nguvu na wanaomuunga mkono Haftar walizuwiya usafirishwaji wa mafuta katika juhudi za kuiwekea shinikizo serikali ya mjini Tripoli inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa.

Deutschland Berlin | Libyen Krieg | General Chalifa Haftar
Jenerali Khalifa HaftarPicha: Getty Images/S. Gallup

Hatua hii ya usitishwaji mapigano inafuatia shinikizo la jumuiya ya kimataifa dhidi ya pande mbili hasimu, kufuatia hofu ya kuzuka upya kwa mapigano kwenye mji wa Sirte. Kila upande umeungwa mkono na makundi yenye silaha na mataifa tofauti ya nje.

Taarifa kutoka pande hizo mbili zimetaka kuondolewa shughuli za kijeshi katika miji ya Sirte na Jufra ulio katikati ya Libya na kutaka uwepo wa polisi watakaosimamia usalama katika miji hiyo.

Hapajatolewa tamko lolote kutoka kwa vikosi vya Haftar, lakini mwezi Juni mbabe huyo wa kivita alikubali pendekezo la Misri la kumaliza mzozo ikiwemo usitishwaji wa mapigano. Tume ya umoja wa mataifa nchini Libya,ilipongeza tamko la usitishwaji mapigano kutoka pande zote mbili na kuomba kuondolewa kwa vikosi vyote vya kigeni na mamluki walioko nchini Libya.

Rais wa Misri, Abdel Fattah El-Sisi pia ameikaribisha hatua hiyo. Kwenye ukarasa wake wa Twitter amesema amepokea tangazo hilo kama hatua muhimu katika kueko na suluhisho ya kisiasa ya mzozo huo. Libya ilitumbukia kwenye machafuko wakati vuguvugu la mwaka 2011 lililoungwa mkono na Jumuiya ya Kujihami ya Nato, lilipomuondoa madarakani aliekuwa rais Muammar Gaddafi, ambae baadae aliuawa.