Papa akamilisha ziara nchini Myanmar na Bangladesh
2 Desemba 2017Papa Francis ambaye ziara yake katika mataifa hayo mawili imeghubikwa na mzozo huo wa Warohingya anajulikana kwa kutetea haki za wakimbizi na mara kwa mara ameelezea kusikitishwa kwake na mateso wanayopitia Warohingya lakini kutokana na sababu za kidiplomasia, hakutaja neno Rohingya hadharani alipowaomba viongozi wa dini ya Kibudha nchini Myanmar kujiepusha na chuki na ubaguzi.
Nchini Bangladesh, alikutana na kundi la wakimbizi wa Rohingya mjini Dhaka. Miongoni mwa wakimbizi waliokutana na Papa ni msichana wa miaka 12 aliyemueleza kuwa amepoteza jamaa zake wote katika shambulizi lililofanywa na wanajeshi wa Myanmar waliposhambulia kijiji chao mapema mwaka huu.
Papa asikitishwa na masaibu ya Warohingya
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani amesema mateso ya Warohingya ni makubwa lakini licha ya kuwa huenda ulimwengu usijali kuhusu masaibu hayo, anaomba msamaha kwa niaba ya wote wanaowatesa Warohingya na kuitaka Jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua zaidi kuumaliza mzozo huo.
Tofauti na nchini Myanmar, Papa amezungumzia wazi wazi masaibu ya Warohingya alipokuwa Bangladesh. Kwa mara ya kwanza katika ziara hiyo iliyodumu kwa siku sita kuanzia Jumatatu, Papa Francis alilitamka neno Rohingya.
Alishauriwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki wa Myanmar kutolitamka ili kuepusha kuzidisha uhasama wa kidini na kuwahatarisha Wakristo nchini humo. Wengi wa watu wa Myanmar ambao ni wa dini ya Kibudha, hawawachukulii Warohingya kuwa raia wa nchi hiyo bali wanadai ni Wabengali kutoka Bangladesh.
Baadhi ya makundi ya kutetea haki za binadamu na wakimbizi wamemshutumu Papa kwa kushindwa kuangazia zaidi mzozo wa Warohingya alipokutana na viongozi wa Myanmar.
Papa Francis hakuzitembelea kambi za wakimbizi, ambako ni wakimbizi wachache waliokuwa wanafahamu kuwa mmoja wa viongozi wenye ushawishi duniani yuko nchini humo kutetea haki zao. Zaidi ya wakimbizi laki sita Warohingya wamekimbilia Bangladesh tangu mwezi Agosti kufuatia operesheni ya kijeshi ambapo inaripotiwa wameuawa, kubakwa na makazi yao kuchomwa.
Myanmar na Bangladesh mwezi uliopita zilitia saini makubaliano ya kuwarejesha nyumbani wakimbizi lakini Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu yana wasiwasi kuwa hali bado si salama kwa wakimbizi hao kurejea katika jimbo la Rakhine.
Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa
Mhariri: Isaac Gamba