Papa Francis ahimiza amani kwa wote Iraq
6 Machi 2021Kiongozi mkuu wa kanisa katoliki duniani Papa Francis anayefanya ziara nchini Iraq,kwa pamoja na kiongozi wa juu wa madhehebu ya Waislamu washia wametoa ujumbe mzito nchini humo wa kuwataka watu waishi pamoja kwa amani.
Katika ujumbe walioutowa leo Jumamosi,viongozi hao wamewatolea mwito waislamu katika nchi hiyo ya kiarabu inayokabiliwa na vita kuikumbatia jamii ya wachache ya Wakristo nchini Iraq iliyoishi katika mazingira magumu kwa kipindi kirefu. Viongozi hao wawili wakuu wa dini mbili tofauti walitowa mwito huo wakati wa mkutano wao wa kihistoria uliofanyika katika mji mtakatifu wa Najaf.
Ulamaa wa juu kabisa wa waislamu washia nchini Iraq, Ayatollah Ali al-Sistani amesema mamlaka za kidini zina jukumu katika kuwalinda wakristo wa nchi hiyo wanaostahili kuishi kwa amani na kufurahia haki sawa na wairaqi wengine. Al-Sistani, mwenye umri wa miaka 90, ni mmoja wa maulamaa wa juu kabisa katika madhehebu ya Shia na ni mara chache sana hujiingiza katika masuala ya kisiasa lakini uingiliaji wake wenye sauti umesaidia kuijenga Iraq ya sasa.
Ni kiongozi mwenye mamlaka na heshima kubwa katika jamii ya Shia ambayo ndiyo madhehebu ya walio wengi nchini Iraq na maoni yake kuhusu masuala ya dini na mengineyo yanazingatiwa na kufuatwa na washia wote ulimwenguni.
Kanisa Katoliki mjini Vatican limesema Papa Francis amemshukuru al-Sistani kwa kupaza sauti yake kuwatetea wanyonge na wenye kukabiliwa zaidi na mateso katika nyakati zilizoshuhudia ghasia kubwa zaidi katika historia ya hivi karibuni nchini Iraq.
Mkutano wa kihistoria baina ya viongozi hao wa dini ulifanyika kweye makaazi ya al-Sistani na ulipangwa kwa miezi kadhaa ambapo kila hatua ilijadiliwa kwa kufanyika mashauriano baina ya pande zote mbili ofisi ya Ulamaa huyo na makao makuu ya Katoliki-Vatican.
Imeelezwa kwamba Jumamosi asubuhi papa Francis mwenye umri wa miaka 84 alielekea kwenye makaazi hayo ya al-Sistani huko Najaf akiwa na msafara wake ambako alipokelewa na kundi la wairaq waliokuwa wamevalia mavazi ya asili. Wakati kiongozi huyo wa kanisa katoliki alipofika eneo la mlangoni waliachiwa njiwa kadhaa weupe kuonesha ishara ya amani.
Na wakati kiongozi huyo akiingia kwenye chumba cha al-Sistani alivua viatu mlangoni. Baada ya mkutano wao uliochukua muda wa takriban dakika 40 papa Francis baadae alikwenda katika mji wa kale wa Ur kushiriki mkutano wa dini mbali mbali uliolenga kuwahimiza Waislamu,wakristo na watu wa imani nyingine nchini Iraq kuweka kando uhasama wao wa muda mrefu na kushirikiana kwaajili ya kuleta amani na mshikamano.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Rashid Chilumba