Papa kuendelea na ziara yake nchini Marekani
22 Septemba 2015Ujumbe huo wa papa Francis kwa waumini wa kanisa hilo unabeba maudhui makubwa mawili ya ziara yake katika mataifa hayo mawili ikilenga kuhamasisha kudumisha maelewano miongoni mwa jamii na pia mahusiano ya kidugu kati ya Cuba na Marekani.
Mara tu baada ya kuwasili nchini Cuba Papa Francis alisema mafanikio yaliyopatikana hadi sasa kuhusiana na hatua ya kurejeshwa kwa mahusiano ya kidemokrasia kati ya Cuba na Marekani kuwa ni mfano wa kipekee wa juhudi za kuleta amani duniani.
Ziara hiyo ya Papa Francis ililenga kutia nguvu katika jitihada zinazoendelea kurejesha mahusiano kati ya mataifa hayo yakiwemo yanayohusu nyanja za kibiashara na pia maswala ya mazingira.
Licha ya maswala hayo kupewa umuhimu wa kipekee na Papa Francis lakini pia yamekuwa ni moja ya vipaumbele vya kanisa Katoliki nchini Cuba.
Kanisa Katoliki lahimiza watu kuheshimu maadili
Hali mbaya ya kiuchumi na hali ya kuhamahama kwa baadhi ya jamiii nchini humo imesababisha kuparaganyika kwa familia nyingi jambo lililopelekea kanisa Katoliki nchini humo kuhimiza juu ya jamii kurejea katika maadili ya asili ya taifa hilo ikiwa ni pamoja na kujituma katika kufanya kazi na pia kuheshimiana miongoni mwao.
Ziara hiyo ya Papa Francis nchini Cuba imekuja katika kipindi muhimu ambacho taifa hilo liko katika mchakato wa maboresho ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na marekebisho katika mifumo yake ya kibiashara ambayo sasa yanalenga kutoa mwanya kwa soko huru na kuipa nguvu sekta binafisi kibiashara kama moja ya mdau wa kukuza pato la taifa hilo.
Papa Francis alikuwa mmoja wa watu waliokuwa mstari wa mbele akiwa ni mpatanishi katika mchakato wa mazungumzo yaliyokuwa yakifanyika kwa siri ya jitihada za kurejeshwa kwa mahusiano ya kidemokrasia na nyanja nyinginezo kati ya Cuba na Marekini.
Mwandishi: Isaac Gamba/APE
Mhariri: Mohammed Khelef