1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Papa Francis alaani huku Iran ikiwahukumu kifo watu watatu

9 Januari 2023

Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, ameungana na viongozi wengine ulimwenguni kulaani kunyongwa washukiwa wa uhalifu kwenye maandamano ya umma nchini Iran, huku wengine watatu wakihukumiwa kifo.

https://p.dw.com/p/4LuPd
Papst Franziskus I Weihnachtsbotschaft „Urbi et Orbi"
Picha: Yara Nardi/REUTERS

Papa Francis alitowa kauli hiyo siku ya Jumatatu (Januari 9) kwenye hotuba yake ya kila mwaka kwa mabalozi wanaowakilisha nchi zao mjini Vatican, ambayo kawaida hutolewa mwanzoni mwa mwaka kuelezea maeneo yanayoangaziwa na sera ya nje ya Kanisa hilo.

Akilinganisha upinzani wa Vatican kwa utoaji mimba na adhabu ya kifo, Papa alisema yote mawili yanavunja haki ya msingi ya kuishi, na kwamba "hayakubaliki kwenye mazingira yoyote."

"Haki ya kuishi pia inahatarishwa mahala ambapo adhabu ya kifo inaendelea kutekelezwa, kama ilivyo sasa nchini Iran, kufuatia maandamano ya kudai haki na heshima zaidi kwa wanawake. Hukumu ya kifo haiwezi kutekelezwa kwa kisingizio cha kulinda haki ya dola, kwani hairejeshi haki hiyo kwa wahanga wala kupunguza machungu yao, bali kuchochea zaidi hasira na visasi." Alisema Papa Francis.

Soma zaidi: Askari wa kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi wa Iran auwawa

Hii ni kauli ya kwanza rasmi kutolewa hadharani na Papa Francis kuhusiana na maandamano yaliyoanza katikati ya mwezi Septemba nchini Iran, kufuatia kifo cha Mahsa Amini, msichana wa miaka 22 aliyepoteza maisha akiwa mikononi mwa polisi ya maadili, waliomshikilia kwa kuvunja sheria za uvaaji za jamhuri hiyo ya Kiislamu. 

Iran yawahukumu kifo wengine watatu

Hotuba ya Papa Francis ilikuja wakati mahakama moja nchini Iran ikiwahukumu kifo watu wengine watatu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya maafisa watatu wa usalama kwenye maandamano hayo.

Iran | Todesurteile | Saeed Yaghoubi, Majid Kazemi und Saleh Mirhashemi
Kutoka kushoto: Saeed Yaghoubi, Majid Kazemi na Saleh Mirhashemi. Wote wamehukumiwa kifo kwa mauaji ya maafisa watatu wa usalama wakati wa maandamano ya kulalamikia kifo cha Mahsa Amini nchini Iran.Picha: Mizan

Hukumu hiyo ya Jumatatu (Januari 9), ambayo bado inaweza kukatiwa rufaa, ilifanya idadi ya waliohukumiwa kifo kufikia 17, wote wakihusishwa na maandamano yaliyodumu kwa zaidi ya miezi mitatu.

Wanne kati ya hao waliohukumiwa wameshanyongwa na wawili wapo kwenye orodha ya kusubiri kunyongwa baada ya rufaa zao kukataliwa kwenye mahakama ya juu. 

Soma zaidi: Iran yamnyonga mtu wa pili kuhusiana na maandamano

Saleh Mirhashemi, Majid Kazemi na Saeed Yaghoubi walihukumiwa kifo kwa kosa liitwalo 'moharebeh' - yaani kutangaza vita dhidi ya Mungu, ambalo kwa mfumo wa sheria nchini humo lina adhabu ya kifo.

Vile vile, wote watatu walikutwa na hatia ya kuwa wanachama wa kundi la kihalifu lenye lengo la kuleta machafuko kwenye nchi, kosa ambalo hukumu yake ni miaka kumi jela.

Wawili wengine walihukumiwa vifungo kwa kushiriki tukio ambalo lilipelekea vifo vya maafisa hao watatu wa usalama katika jimbo la Isfahan, mnamo tarehe 16 Novemba.

Mmoja wao ni mcheza soka maarufu, Amir Nasr-Azadani, mwenye umri wa miaka 26, ambaye amehukumiwa miaka 26 jela kwa makosa matatu, likiwemo la kusaidia kosa la 'moharebeh'.

Vyanzo: AFP/AP/Reuters