1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPapua New Guinea

Papa Francis arai utajiri uwanufaishe wote Papua New Guinea

7 Septemba 2024

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis ameanza ziara yake nchini Papua New Guinea leo ambako ametoa mwito wa kutumiwa rasimali kubwa inayopatikana kwenye taifa hilo kwa manufaa ya "jamii nzima".

https://p.dw.com/p/4kO3l
Papa Francis
Papa Francis Picha: Tatan Syuflana/AP Photo/picture alliance

Akiwahutubia viongozi wa kiiasa na wafanya biashara, baba mtakatifu Francis amesema ni muhimu kwa maliasili zinazopatikana Papua New Guinea ikiwemo madini, vito vya thamani na gesi asilia viwanufaishe watu wote.

Matamshi yake yumkini yatachochea mjadala kwenye taifa hilo la kanda ya Pasifiki ambalo wengi ya raia wake wanaamini utajiri wao unawanufaisha wachache kwa njia za wizi na ufisadi.

Licha ya utajiri mkubwa wa maliasili, Papua New Guinea ndiyo nchi masikini zaidi kwenye kanda hiyo na kati ya robo hadi nusu ya raia wake milioni 12 wanaishi kwenye umasikini uliotopea.