1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSudan Kusini

Papa Francis awasili nchini Sudan Kusini

Hawa Bihoga
3 Februari 2023

Papa Francis amewasili nchini Sudan Kusini akitokea nchini Kongo Ijumaa, katika ziara yake ya siku tatu inayolenga kuhimiza amani na maridhiano

https://p.dw.com/p/4N4ma
Pope Francis visits South Sudan
Picha: Vatican Media/REUTERS

Papa Francis anatarajiwa kuhimiza amani na maridhiano katika nchi hiyo changa zaidi duniani lakini inayokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe pamoja na umasikini uliokithiri.

Papa Francis akiwa kwenye kiti chake cha magurudumu, alilakiwa na viongozi mbalimbali wa Sudan Kusini akiwemo Rais Salva Kiir.

Ziara ya papa iliotafsiriwa kama hija, ni ya kwanza nchini humo tangu taifa hilo lenye Wakristo wengi kupata uhuru kutoka kwa Sudan yenye Waislamu wengi mwaka 2011 baada ya miongo kadhaa ya migogoro.

Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliodumu kwa miaka mitano yameuwa watu 380,000, na wengine milioni 4 wameyakimbia makaazi yao huku taifa hilo likisalia kwenye umasikini.

Papa Francis anatarajiwa kukutana na waathirika wa mapigano hayo, viongozi wa kisiasa na makanisa katika misa ya wazi inaotarajiwa kukusanya umati mkubwa.