Papa Francis awataka Wakongo kusamehe
1 Februari 2023Amesema hayo leo alipoongoza ibada iliyohudhuriwa na zaidi ya waumini milioni moja mjini Kinshasa, kwenye taifa hilo ambalo limezongwa na machafuko kwa miongo mingi.
Akizungumzia miongo mingi ya machafuko ambayo yamewasababisha mamilioni kukimbia makwao hususan mashariki mwa nchi hiyo, Papa Francis alisisitiza kwamba kusamehea sio kujifanya kwamba hakuna maovu ambayo yamefanyika, bali tendo hilo hukuza msamaha moyoni.
"Katika ulimwengu ambao umejaa machafuko na vita, Wakristo sharti wawe kama Yesu. Kama kusisitiza hoja hiyo, Yesu alisisitiza hilo kwa wanafunzi wake kuwa amani iwe nanyi!" Alisema mbele ya umati wa watu wapatao milioni moja.
Waumini wengi walikesha katika uwanja wa ndege wa Ndolo wamkisubiri Papa Francis kuongoza misa hiyo, na alipowasili walimpokea kwa nyimbo, densi na msisimko mkubwa.
Ziara hiyo ni ya kwanza ya kipapa kufanyika nchini humo tangu mwaka 1985, wakati papa wa zamani, marehemu John Paul wa Pili, alipoizuru Kongo.