1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiSudan Kusini

Papa Francis kukutana na wahanga wa vita Sudan Kusini

4 Februari 2023

Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani Papa Francis leo Jumamosi atakutana na wahanga wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan Kusini katika siku ya pili ya ziara yake kwenye taifa hilo linalokabiliwa na machafuko.

https://p.dw.com/p/4N5tf
DR Kongo | Papst Franziskus in Kinshasa
Picha: Arsene Mpiana/AFP/Getty Images

Mkutano huo unafuatia wito alioutoa Papa Francis siku ya Ijumaa kwa viongozi wa Sudan Kusini akiwataka kutafuta amani ya kudumu na kukomesha mateso yanayowakumba raia. 

Papa Francis aliyewasili nchini Sudan Kusini Ijumaa Alasiri akitokea Kongo, amefanya mazungumzo na rais Salva Kiir wa nchi hiyo hapo jana na kutoa wito wa amani.

Papa Francis amewataka viongozi wa taifa hilo changa kupambana bila kuchoka kusaka amani na kumaliza machafuko nchini humo yanayosababisha madhila ya kila siku kwa raia.

Baba Mtakatifu amekaririwa akimweleza rais Kiir "hakuna tena nafasi ya kufanywa uharibifu" na badaa yake taifa hilo lienze kazi hivi sasa ya kujijenga.

Rais Kiir alikuwa pamoja na hasimu wake wa muda mrefu ambaye ni makamu wa rais wa nchi hiyo Riek Machar wakati alipomkaribisha Papa Francis kwenye bustani ya ikulu ya rais mjini Juba.

Papa Francis awataka mafahali wawili wa Sudan Kusini kufanikisha amani 

Pope Francis visits South Sudan
Papa Francis alipolakiwa na rais Salva Kiir katika Ikulu ya Sudan Kusini mjini JubaPicha: Vatican Media/REUTERS

Kiongozi huyo wa kiroho amewarai viongozi hao hadharani wafanya pamoja kukomesha umwagikaji wa damu, machafuko na uhasama.

Rais Kiir na hasimu wake Machar walikuwa wageni wa Papa Francis mjini Vatican mnamo mwaka 2019 na wakati huo baba mtakatifu aliwanasihi kuisaka amani na alionesha kitendo cha heshima kubwa kwa kuibusu miguu ya wanasiasa hao wawili.

Kiir na Machar walifanikiwa baadaye kufikia makubaliano ya amani lakini yalisambaratika na machafuko yakazuka upya kwenye taifa hilo changa la Afrika Mashariki.

Kwenye mazungumzo na viongozi hao Papa Francis alipendekeza "njia mpya" ya kuharakisha mchakato wa maridhiano. Amewatolea mwito wanasiasa hao kuzuia kuingizwa kwa silaha nchini Sudan Kusini akisema taifa hilo linahitaji vingi vya muhimu badala ya zana za maangamizi.

Pia alipigia upatu umuhimu wa kuimarishwa kwa sera za afya na miundombini ya taifa hilo. Sudan Kusini mara kadhaa imeorodheshwa kuwa moja ya mataifa masikini zaidi ulimwenguni.

Miaka chungunzima ya vita vya wenyewe kwa wenye imewaacha raia wake katika hali ngumu ya maisha huku wakikosa huduma za msingi za jamii.

Je, ziara ya kiongozi wa kiroho itawapatia raia wa Sudan Kusini ahueni?

Rais Kiir ameahidi kuanzisha tena kile kinachofahamika kuwa mazungumzo ya mjini Roma pamoja na makundi ya waasi ambao hawautambui mkataba wa amani uliotiwa saini. Amesema anatumai wabunge wa nchi hiyo kutoka upande wa upinzani watamuunga mkono kufanikisha upatikanaji amani.

Kuelekea ziara ya Baba Mtakatifu, raia nchini Sudan Kusini walikuwa na matumaini makubwa kuwa kiongozi huyo wa kiroho atasaidia kupunguza mivutano inayoligubika taifa hilo.

DR Kongo | Papst Franziskus in Kinshasa
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Licha ya kuwepo utulivu ndani ya serikali, bado kumewaka na matukio ya machafuko yanayozuka mara kwa mara ndani ya nchi hiyo.

Ziara ya Papa Francis imevutia watu kutoka kila pembe ya nchi hiyo ambao wamesafiri hadi kwenye mji mkuu Juba, wengi wakiwa na matumaini ya kushuhudia kuhuishwa kwa wito wa kuwepo amani.

"Ninatamani ziara hii iwe mwanzo wa amani na utulivu" amesema James Oyet Latansio ambaye ni katibu wa Baraza la Makanisa nchini Sudan Kusini. Hata hivyo, saa kadhaa kabla Papa Francis kukanyaga ardhi ya Sudan Kusini, kulikuwa na wimbi la machafuko lililosabbaisha vifo vya takribani watu 20.

Kwenye ziara hiyo Papa Francis amefuatana na Askofu Mkuu wa Canterbury na mkuu wa kanisa la Anglikana  Justin Welby, na kiongozi wa kanisa la Scotland Iain Greenshields.

Ziara hii inayoitwa iliyopewa jina la "Hija ya amani" ni ziara ya kwanza kabisa ya Papa Francis nchini Sudan Kusini tangu taifa hilo lenye Wakristo wengi kupata uhuru kutoka kwa Sudan yenye Waislamu wengi mwaka 2011 baada ya miongo kadhaa ya migogoro.