1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis: Madai ya wanawake ni halali kutaka haki zaidi

Zainab Aziz Mhariri: Sekione Kitojo
2 Aprili 2019

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amesema wanawake wana madai halali ya kutaka usawa katika Kanisa lakini alisita kuidhinisha miito ya moja kwa moja kutoka kwa maaskofu wake juu ya mabadiliko makubwa.

https://p.dw.com/p/3G6rI
Marokko Papstbesuch | Messe in Sportzentrum Prince Moulay Abdellah in Rabat
Picha: Getty Images/AFP/A. Pizzoli

Papa Francis amesema hayo katika waraka wake mrefu unaoitwa Yesu bado yuko hai lakini hakuidhinisha hitimisho kama  hilo. Papa Francis amesema Kanisa linalowasikiliza vijana linapaswa pia kuyazingatia madai halali ya wanawake juu ya haki na usawa. Ameeleza kuwa Kanisa lina jukumu la kutoa mafunzo mazuri zaidi kwa wanaume na wanawake wenye uwezo wa kuongoza.

Waraka uliyotolewa na Papa Francis, kwa ajili ya vijana wakatoliki wa leo inatokana na mkutano wa maaskofu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka uliopita ambapo maaskofu hao walijadili njia bora ya kuwahudumia vijana. Suala la utashi wa haki zaidi kwa wanawake lilikuwa la kipaumbele kwenye mkutano huo. Katika azimio lao maaskofu walitoa wito kutaka wanawake wapewe nafasi za uongozi na mamlaka ya kushiriki katika  kupitisha maamuzi ya Kanisa. 

Katika hati yake Papa Francis amesema Kanisa linapaswa kuiangalia historia yake na kutambua kwamba pamekuwepo udikteta wa wanaume,utumwa wa aina mbalimbali na unyanyasi wa kingono na kutokana na hayo anaweza kuunga mkono miito juu ya kuheshimu zaidi haki za wanawake na pia kuunga mkono usawa baina ya wanawake na wanaume licha ya kutokubaliana na hoja zote zinazotolewa na watetezi wa haki za akina mama.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa FrancisPicha: Getty Images/AFP/F. Senna

Akizungumza na waandishi habari juu ya kutozingatiwa suala la mashoga katika hati ya Papa Francis, mwandalizi wa mkutano wa maaskofu, Kadinali Lorenzo Baldsseri ameeleza kuwa baba mtakatifu amekiri katika hati yake kwamba hawezi kuandika upya kila kitu.

Katika waraka wake Papa Francis alihamasishwa na mapendekezo muhimu zaidi yaliyotolewa kwenye mkutano wa maaskofu. Hati ya kiongozi wa kanisa katoliki inazingatia masuala mbalimbali yanayowakibili vijana wa leo na kutilia maanani kwamba vijana wengi wanahisi kutengwa na Kanisa Katoliki kutokana na kashfa za unyanyasi wa kingono na ufisadi wa fedha na kwamba vijana hao wenyewe wanasibika kutokana na kukandamizwa, migogoro na hali ya kukata tamaa.

Papa Francis ametoa wito wa kuleta mageuzi ya haraka kwenye shule za wakatoliki na mafunzo ya ukasisi na kueleza kwamba aghalabu mafunzo hayo yanatuama katika ubinafsi na kuwaepusha vijana na makosa ya dunia bila ya kuzingatia hali halisia za maisha ya vijana.

Juu ya udhalilishaji wa kingono Papa Francis ametoa wito wa kuung'oa mfumo wa mamlaka ambao umekuwa unatumika ndani ya Kanisa uliowezesha uhalifu huo kutendeka. Pia ametaka kuikabili changamoto kuhusu viongozi wa Kanisa waliivyoishughulikia mikasa ya unyanyasi kwa uzembe na bila ya uwazi.

Kiongozi wa Kanisa Katoliki diniani amesema mbegu ya ufisadi inatokana na uroho wa mamlaka,ukosefu wa mdahalo,uwazi,maisha ya undumilakuwili na pia inatokana na utovu wa imani na udhaifu wa kimawazo. Amewataka waumini kuwakemea makasisi wanaotaka kujiburudisha kwa kuwadhulumu vijana na kuwakumbusha wajibu wao kwa Mungu na kwa watu wao.

Vyanzoz/AP/RTRE