1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis : Siasa za kizalendo ni kitisho kwa demokrasia

4 Desemba 2021

Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Francis ametahadharisha juu ya kitisho cha siasa za itikadi kali za mrengo wa kulia akisema zinaiweka rehani demokrasia barani Ulaya.

https://p.dw.com/p/43qEl
Griechenland | Besuch Papst Franziskus
Papa Francis akiwa ziarani nchini UgirikiPicha: Alessandra Tarantino/AP Photo/picture alliance

Akiwasili nchini Ugiriki, chimbuko la demokrasia duniani, Papa Francis amesema "majawabu mepesi" yanayotolewa na wanasiasa wa mrengo mkali wa kulia ni janga kwa demokrasia na kutoa wito wa kuweko dhamira mpya ya pamoja ya kuhimiza mwelekeo sahihi.

Kiongozi huyo wa kiroho ameitumia hotuba yake mbele ya viongozi wa kisiasa na kitamaduni nchini Ugiriki kutoa tahadhari kwa Ulaya kuhusu vitisho vinavyolikabili bara hilo linapokuja suala la siasa za hamasa.

Amesema kushiriki kwa mataifa yote duniani ndiyo kunaweza kutatua masuala nyeti yanayoukabili ulimwengu ikiwemo kuyalinda mazingira, kupambana na janga la virusi vya corona na hata umasikini.

"Hapa ndiyo demokrasia ilizaliwa" alisema Papa Francis akimwambia rais wa Ugiriki Katerina Sakellaropoulou na kufafanua wasiwasi alio nao juu ya hatma ya demokrasia barani Ulaya.

"Siasa inahitaji hili, ili kuweka maslahi ya pamoja mbele badala ya maslahi binafsi" amesema Papa Francis na kukumbusha kuwa Ulaya na ulimwengu hauwezi kupuuza hali ya kuanguka kwa misingi ya demokrasia duniani.

Mivutano ya kiimani yashuhudiwa wakati wa ziara ya Papa

Griechenland | Besuch Papst Franziskus
Picha: Vatican Media/REUTERS

Akianza ziara yake ya siku  nchini Cyprus na Ugiriki Papa Francis alikumbusha kwamba ilikuwa ni Ugiriki, ambayo kulingana na mwanafalsafa Aristotle, ndiye iligundua kuwa binadamu ni kiumbe chini ya mfumo wa siasa unaotambua kuwa haki na umuhimu wa ustawi wa wengine

Jumamosi jioni, Papa Francis alikutana na kiongozi wa kanisa la Orthodox nchini Ugiriki, Askofu Mkuu Ieronymos.

Akiwasili kwenye eneo hilo kasisi mmoja wa kanisa la Orthodox alipayuka maneno "Papa, wewe ni mzushi" katika tukio ambalo kiongozi huyo wa kidini hakulipa umuhimu linakumbusha mivutano ya kiimani iliyopo kati ya wakristo wa madhehebu ya kiorthodox na kikatoliki nchini Ugiriki.

Historia ya maisha ya Papa Francis na umuhimu wa demokrasia

Zypern Papst Franziskus und Präsident Anastasiades
Papa Francis pi aliitembelea Cyprus katika ziara yake ya siku tanoPicha: IAKOVOS HATZISTAVROU/AFP

Papa Francis ambaye aliishi chini ya enzi ya utawala wa siasa  za kizalendo nchini Argentina na udikteta wa kijeshi, mara kadhaa ameonya juu ya tawala za kiimla na siasa za hamasa zinavyotishia ustawi wa kanda ya Umoja wa Ulaya na demokrasia kwa jumla.

Ingawa hakutaja majina ya nchi au viongozi wakati wa hotuba yake, lakini Umoja wa Ulaya ungali kwenye mkwamo na nchi wanachama Poland na Hungary juu ya masuala ya utawala wa sheria ambapo Poland inasisitiza kuwa sheria za nchi hiyo zina nguvu kushinda sera na kanuni za Umoja wa Ulaya.

Nje ya kanda hiyo, viongozi wa siasa za kizalendo nchini Brazili na hata rais wa zamani wa Maekani Donald Trump walitekeleza sera za kujali mataifa yao pekee katika masuala mfano wa mazingira jambo linalokwenda kinyume na mwito wa Papa Francis anayehimiza ushirikiano wa pamoja duniani.