Papa Francis ziarani Iraq
5 Machi 2021Ndege ya Italia iliyombeba Papa Francis, imeondoka leo mjini Roma na inatarajiwa kuwasili muda wowote katika mji mkuu wa Iraq, wa Baghdad. Iraq imesambaza maelfu ya maafisa wa ziada wa usalama kwa ajili ya kumlinda Papa Francis wakati wa ziara yake, ambayo inakuja baada ya mkururo wa mashambulizi ya maroketi na mabomu ya kujitoa muhanga na hivyo kuibua wasiwasi juu ya usalama wa kiongozi huyo.
Wakati wa ziara yake Papa Francis ataitembelea miji minne ikiwemo mji wa zamani uliokuwa ngome ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS wa Mosul, ambako makanisa na majengo mengine bado yamebeba makovu ya mzozo wa nchi hiyo. Akiwa mjini Mosul atakutana na jamii ndogo ya Wakristo waliorejea Qaraqosh.
Pia atatembelea eneo la Ur, ambalo ni mahali alikozaliwa mtume Abraham anayeaminiwa na Wakristo, Waislamu na Wayahudi na pia kukutana na kiongozi mkuu wa Waislamu wa kishia Ayatollah Ali al-Sistani katika mji wa kusini wa Najaf.Papa Francis awasili Thailand
Mkutano wake na Sistani ambaye ana ushawishi mkubwa katika siasa za Iraq na jamii kubwa ya Washia, ni wa kwanza kufanywa na Papa. Baadhi ya makundi ya wanamgambo wa kishia yamepinga ziara hiyo ya Papa, yakiitaja kuwa uingiliaji wa mataifa ya magharibi katika masuala ya Iraq. Lakini Wairaq wengi wanatumai ziara hiyo itasaidia kukuza mtizamo mpya wa Iraq.
Papa Francis ataendesha ibada katika kanisa la mjini Baghdad ambalo lilikuwa moja ya eneo la mauaji mabaya ya wakristo katika mashambulizi ya wanamgambo mwaka 2010, ambapo watu 58 walipoteza maisha.
Katika ujumbe wake alioutoa jana kwa njia ya video, Papa Francis aliwaeleza watu wa Iraq kuwa anakwenda kama "hujaji wa amani" anayetafuta "undugu".
"Ninakuja kama hujaji, hujaji anayekusudia kuomba msamaha wa Mungu na upatanisho baada ya miaka ya vita na ugaidi, kumwomba Mungu faraja ya mioyo na uponyaji wa majeraha. Ninakuja kama hujaji wa amani."
Ziara yake inakuja wakati Iraq ikishuhudia ongezeko la maambukizi mapya ya virusi vya corona hususan yanayotokana na aina mpya ya kirusi. Kiongozi huyo na ujumbe wake wote wamepatiwa chanjo kabla ya safari.Kiongozi wa Kanisa katoliki Papa Francis ziarani Japan
Wakati mmoja kulikuwa na idadi ndogo ya Wakristo nchini Iraq, lakini idadi yao ilipungua baada ya uvamizi wa mwaka 2003 ukiongozwa na Marekani na baadae idadi hiyo ilipungua zaidi wakati wapiganaji wa IS walipoidhibiti miji iliyokuwa ikikaliwa na wakristo. Kufikia mwaka 2003 kulikuwa na Wakristo milioni 1.4 nchini humo na hivi sasa idadi yao inakadiriwa kuwa 250,000.