1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis asema dunia hivi sasa inaonekana kukosa amani

Admin.WagnerD28 Julai 2016

Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis amesema ulimwengu hivi sasa uko katika vita huku akisisitiza kuwa vita hiyo haisababishwi na dini wakati alipowasili nchini Poland .

https://p.dw.com/p/1JX65
Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis akisalimia baada ya kuwasili nchini Poland.
Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis akisalimia baada ya kuwasili nchini Poland.Picha: Reuters/D.-W. Cerny

Hayo ni maneno aliyosikika akiyatamka Kiongozi huyo mkuu wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis alipokuwa akiwasalimia waumini wa kanisa hilo mara baada ya kuwasili nchini humo.

Katika hotuba yake ya kwanza mara tu baada ya kuwasili katika jiji la Krakow nchini Poland baba mtakatifu alisema njia ya kukabiliana na hofu inayoweza kujitokeza ni kuwa tayari kuwapokea wakimbizi wanaokimbia migogoro na mazingira magumu katika nchi wanazotoka.

"Kufungua milango kwa wahamiaji inahitaji busara na moyo wa huruma" alisikika Papa Fransis akionekana kutofurahishwa na serikali zinazofuata siasa za mrengo wa kulia ambazo ziligoma kuwapokea wakimbizi wakati wa mgogoro mkubwa wa wakimbizi barani ulaya tangu kumalizika kwa vita kuu vya pili vya dunia.

Asema ulimwengu uko katika hali ya vita

Papa Francis alisema hatupaswi kuogopa kusema ukweli na kuongeza kuwa ulimwengu hivi sasa uko katika hali ya vita kwa sababu amani imepotea. " Wakati napozungumzia vita namaanisha ni mapambano dhidi ya masilahi, pesa na rasilimali na siyo dini, kwani dini zote zinataka amani, bali wengine ndio wanapenda vita " alisema kiongozi huyo mkuu wa kanisa Katoliki duniani.

Polen Weltjugendtag 2016 in Krakau Papst Franziskus und Andrzej Duda
Picha: picture alliance/dpa/G. Momot

Tukio la mauaji ya kikatili dhidi ya kasisi wa kanisa Katoliki wakati wa misa nchini Ufaransa jumanne ya wiki hii katika shambulizi linalodaiwa kufanywa na kundi la itikadi kali la Dola la Kiisilamu linaonekana kugonga vichwa vya habari kuhusiana na ziara hiyo ya Papa Francis nchini Poland mnamo wakati kongamano la kimataifa la siku ya vijana wa kanisa Katoliki likifanyika nchini humo.

Baba Mtakatifu alisema dunia ilikuwa katika hali ya vita kwa wakati fulani akimaanisha vita ya dunia ya mwaka 1914, na vita ya pili ya dunia katika kipindi cha kuanzia mwaka 1939 hadi mwaka 1945 na sasa kuna vita hii.

Mfululizo wa mashambulizi yanayowalenga raia barani ulaya umeonekana kupunguza idadi ya washiriki katika tamasha hilo la wiki moja la kidunia la vijana wa kanisa Katoliki.

Kundi la vijana waliokuwa wakipeperusha bendera walijitokeza mbele ya kiongozi huyo wa kidini na kumshangilia pasipo hata kuhofia usalama wao .

" Nimefanikiwa kumuona Papa Francis alikuwa mita tano mbele yangu, ni vema kumuona mtu wa aina yake ana kwa ana na siyo kumuona tu katika televisheni." alisikika kijana mmoja wa Kipoland Karina Borowicz.

Kiasi ya waumini wa kanisa hilo wapatao 200,000 walishiriki misa ya ufunguzi wa tamasha hilo la vijana kinyume na matarajio ya idadi ya watu karibu nusu milioni ambao walitarajiwa kushiriki misa hiyo.

Tukio la kuuawa kwa kasisi wa kanisa hilo nchini Ufaransa limeonesha kutia doa harakati za Papa Francis za kupenyeza hoja ya kupokelewa kwa wakimbizi mnamo wakati akitumia nguvu yake ya ushawishi kumataka Waziri Mkuu wa Poland Beata Szydlo na serikali yake ya mrengo wa kulia ambayo imekataa kuwapokea wakimbizi kwa sababu za kiusalama.

Papa Francis katika mazungumzo na Rais wa Poland Andrezej Duda
Papa Francis katika mazungumzo na Rais wa Poland Andrezej DudaPicha: picture alliance/dpa/P. Supernak

Hata hivyo Rais wa Poland Andrezej Duda aalionyesha dalili za kuregeza msimamo huo wa Poland kufuatia kikao cha ndani kati yake na Papa Francis.

"Kama kuna mtu anataka kuja nchini humu hasa kama ni wakimbizi wanaokimbia mapigano tutawapokea " alisema kiongozi huyo alipozungumza na waandishi wa habari.

Poland iko katika hali ya tahadhari ya kiusalama, ikiwapokea zaidi ya wageni 40,000 kwa ajili ya tamasha hilo huku mamlaka za nchi hiyo ikimtia mbaroni raia mmoja wa Iraq kwa kukutwa na idadi kadhaa ya vilipuzi.

Mwandishi : Isaac Gamba / AFPE

Mhariri :Hamidou Oummilkhheir