Paul Kagame-Kiongozi mwenye maono, dikteta au vyote?
1 Agosti 2017Paul Kagame anatukuzwa kwa kusitisha mauaji ya kimbari nchini Rwanda na kuielekeza nchi hiyo katika kile wale wanaomsifu wanakiita maajabu ya kiuchumi, lakini wakosoaji wake wanamuona kama dikteta , mtawala mwenye mamlaka yote ambaye anaukandamiza upinzani na anatawala kwa kuleta hofu.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 59 mpiganaji wa zamani wa chini kwa chini anawania muhula wa tatu madarakani katika uchaguzi wa hapo Ijumaa Agosti 4 baada ya wapiga kura kuidhinisha kwa wingi mabadiliko ya katiba ili Kagame agombea tena na kubakia madarakani kwa miongo mingine miwili.
Kagame anasema hatua yake ya kuwania madaraka ni wajibu kwa nchi yake, hata hivyo hatua hiyo imewakasirisha washirika wa kimataifa ambao uvumilivu wao unavikia mwisho kwa mtu huyo ambaye alikuwa akionekana kama mfano wa mafanikio katika uongozi wa bara la Afrika baada ya kipindi cha ukoloni.
Hata hivyo rais wa nchi hiyo ndogo ya Afrika ya kati amekuwa mmoja katika viongozi wenye nguvu kabisa katika bara la Afrika na wanaosifiwa sana. Wenzake , wanatiwa hamasa na mabadiliko nchini Rwanda , wamempa jukumu la kubadilisha Umoja wa Afrika.
Mauaji ya kimbari
Nchi hiyo iliyovurugika kutokana na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 na bila ya kukuta kipande cha ndururu ya fedha katika hazina ya taifa Kagame aliingia madarakani, na Rwanda hivi sasa inaukuaji wa uchumi unaofikia kwa wastani wa asilimia 7 kwa mwaka wakati mji mkuu Kigali umebadilika na kuwa mji mkuu wenye majengo mazuri, safi, mitaa salama na kutokuvumilia kabisa rushwa.
"Kagame anafahamika kuwa ni mchapa kazi na mtekelezaji, na sio mtu ambaye anasema mambo tu kama watu wengine," amesema Desire Assogbavi , mratibu wa shirika la Oxfam katika Umoja wa Afrika ambaye anaandika mara kwa mara katika blogu yake kuhusu taasisi hiyo ya Afrika.
Rafiki wake wa karibu Tony Blair anamsifu kuwa ni "kiongozi mwenye maono" kutokana na maendeleo makubwa aliyoiletea nchi yake.
Wajihi wa rais huyo , unaoelezwa kuwa "dikteta asiye na msamaha" na mwandishi Philip Gourevitch , ambaye aliandika maenezo mazito juu ya mauaji ya kimbari, ulitengenezeka wakati akikua uhamishoni.
Uhamishoni
Mwaka 1960, wakati akiwa na umri wa miaka mitatu , familia yake ya jamii yenye uwezo ya Watutsi ilikimbilia katika nchi jirani ya Uganda ikikimbia mauaji ya halaiki nchini mwao.
Akitumikia jeshi la waasi waliokuwa wakiongozwa na rais Yoweri Museveni kabla na baada ya kukamata madaraka mwaka 1986, alipanda na kuwa mkuu wa kitengo cha usalama wa taifa.
Kagame ambaye ni rais pekee anafahamika kupata mafunzo ya kijeshi nchini Marekani na Cuba, baadaye alichukua uongozi wa kikundi kidogo cha waasi wa Rwanda wanaoishi uhamishoni ambao walijipenyeza ndani ya Rwanda wakitarajia kuiangusha serikali ya rais Juvenal Habyarimana mwaka 1990, na kuzusha vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Kifo cha Habyarimana katika ajali ya ndege kilizusha miezi mitatu ya mauaji ya kimbari mwaka 1994, wengi wao wakiwa Watutsi waliouwawa na vijana wa Kihutu ambao ni kabila lenye watu wengi nchini humo wakihimizwa na kauli za chuki.
Kagame baba wa watoto wanne, alikuwa na umri wa miaka 36 wakati huo jeshi la wasi wa Rwandan Patriotic Front RPF lilipoyafurusha majeshi ya Rwanda ambayo yaliwauwa watu wanaokadiriwa kufikia 800,000 na kuukamata mji mkuu Kigali, na kuwa kiongozi rasmi wa nchi hiyo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Mohammed Khelef