1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pazia la kuchukua fomu za ugombea lahitimishwa Chadema

6 Januari 2025

Pazia la uchaguzi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema kwa wagombea wake kuchukua na kurejesha fomu limefungwa na kwamba sasa imefahamika rasmi kambi mbili zitachuana katika uchaguzi huo.

https://p.dw.com/p/4oqvs
Tansania Daressalam 2024 | Führung der Oppositionspartei CHADEMA bei Treffen
Viongozi wa chama cha upinzani Tanzania CHADEMA, Tundu Lissu, makamu mwenyekiti na mwenyekiti Freeman Mbowe, wakiwa kwenye mkutano jijini Dar es Salaam. Tarehe: 10.12.2024Picha: Eric Boniface/DW

Uchaguzi nkuu wa Chadema utafanyika Januari 21. Kama kuchanga karata za kisiasa hakuna ajuaye moja kwa moja kwamba mwenyekiti anayetetea nafasi yake, Freeman Mbowe au mpinzani wake katika nafasi hiyo, Tundu Lissu amefanikiwa.

Hata hivyo, mazingira ya kisiasa ndani ya chama chenyewe yanaonyesha kuna upande mmoja umecheza mchezo wenye kuashiria mengi.

Mwanasisasa Jonh Heche na hatua ya kumuunga mkono mgombea Lissu

Tansania Daressalam | Rückkehr des früheren Präsidentschaftskandidaten Tundu Lissu
Naibu Mwenyekiti Tundu Lissu akiwampungia mkono wafuasi wake alipowasili Dar es Salaam, Tanzania, Januari 25, 2023.Picha: Eric Boniphace/DW

Zaidi hatua ya mwanasiasa wa muda mrefu wa chama hicho, John Heche kujitokeza katika dakika za mwisho mwisho kuchukua fomu kuwania nafasi ya makamu mwenyekiti Tanzania bara huku akitangaza kumuunga mkono mgombea wa uenyekiti Tundu Lissu imekoleza mjadala kuhusu uchaguzi huo.

Katika hali ya kujiamini, Heche ametangaza kumstaafisha bosi wake Mbowe akisema Chedema itazaliwa upya ndani ya safu mpya ya uongozi.

Mbowe aliyeongoza nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka 15 anaungwa mkono na kambi kadhaa za kikanda na karata yake inasukumwa na mgombea wa nafasi ya makamu mwenyekiti, Ezekiel Wenje ambaye katika siku za hivi karibuni alitumbikia katika sasa za kurushiana tuhumu na mgombea wa kambi ya pili Tundu Lissu.

Matarajio ya ushindi kwa kwa pande hasimu

Kambi ya Lissu imeanza kujinasibu kushinda uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Januari 21 lakini haijaweka bayana namna itakavyoukamata ushindi huo.

Wakati huu kambi ya Mwenyekiti Mbowe inatajwa kuanza kutafakari jinsi ya kukabiliana na wapinzani wake ambao wanaonekana kufanya uamuzi wa kushtukiza kuwania nafasi za juu za chama hicho.

Kambi zote hata hivyo, zimejenga ushawishi ndani ya chama kuanzia ngazi huko mashinani hadi katika vikao vikuu vya chama hicho. Swali linaloendelea kuumiza vichwa wachunguzi wa mambo ni kwa kiasi gani chama hicho kitafanikiwa kufanya uchaguzi wake na hatimaye kuvuka salama bila kulizamisha jahazi la chama.

Soma zaidi:Lissu atoa wito uchaguzi wa Chadema ufanyike kwa uwazi

Yule atayefanikiwa kuongoza jahazi la chama hicho, moja ya mtihani wake wa kwanza ni kujenga umoja wa chama na kisha kuendelea kusukuma mbele ushawishi wa chama kwa wananchi kuelekea katika uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu