1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pedro Sanchez anatarajiwa kuwa Waziri mkuu wa Uhispania

Shisia Wasilwa
1 Juni 2018

Kiongozi wa chama cha Kisoshalisti nchini Uhispania Pedro Sanchez anatarajiwa kuwa Waziri mkuu mpya  baada ya hasimu wake wa kisiasa wa muda mrefu Mariano Rajoy kushindwa bungeni kwenye kura ya kutokuwa na imani naye.

https://p.dw.com/p/2yoMJ
Spanien | Parlamentsdebatte zum Misstrauensvotum gegen Ministerpräsident Rajoy | Pedro Sanchez
Picha: Reuters/S. Perez

Sanchez mwenye umri wa miaka 46 ameahidi kufanya mazungumzo na viongozi wanaotisha kujitenga kwa jimbo la  Catalonia.

Sanchez  kiongozi wa PSOE, aliwasilisha hoja ya kutokuwa na imani na Rahoy  baada ya kashfa ya ufisadi iliyohusisha chama cha Rajoy cha People's Party (PP).

Hatua hiyo huenda ni enzi mpya kwa taifa lenye uchumi wa nne kwa ukubwa katika Umoja wa Ulaya lililoongozwa na chama cha kihafidhina chini ya Waziri mkuu  Rajoy tangu mwaka mwaka 2011.

Wakati akiwa katika upinzani, Sanchez — profesa wa zamani wa uchumi — alipinga vikali mipango ya kupunguza gharama za matumizi iliyoanzishwa na wahafidhina na kuahidi kuongeza  matumizi kwa maslahi ya raia.

Mtazamo mpya wa Catalonia:

Sanchez ameahidi kuanzisha mazungumzo na serikali ya Catalonia kuhusu mzozo wa kutaka kujitenga jimbo hilo  ambapo Uhispania ilitumia nguvu kutaka kumtia nguvuni  kiongozi wa jimbo hilo Carles Puigdemont aliyeitoroka nchi hiyo. Mbali na hayo, Sanchez amehimiza mageuzi ya kikatiba kuanzisha mfumo wa shirikisho ambao utaifanya  Catalonia  ibakie  ndani ya Uhispania.

Bunge Uhispania
Bunge la Uhispania Picha: Getty Images/AFP/O. del Pozo

Hata hivyo, kiongozi huyo wa Kisoshalisti pia alionekana pamoja na Rajoy kwenye Televisheni mwezi Mei, akithibitisha haki ya serikali ya Uhispania kuingilia kati iwapo mrithi wa Puigdemont, Quim Torra atakiuka katiba. Mwezi Mei, 2018, alimlinganisha Torra kuwa sawa na Kiongozi wa Chama cha siasa kali za Kizalendo nchini Ufaransa Marien Le Pen, akimwita "Le Pen wa siasa za Uhispania."

Kuunga mkono Umoja wa Ulaya:

Licha ya kuukosoa mpango wa kupunguza matumizi, Sanchez hajaficha msimamo wake kuhusu Umoja wa Ulaya ama uanachama wa Uhispania katika Umoja wa Ulaya. Pia ameahidi kuzingatia bajeti ya kitaifa iliyopitishwa chini ya Rajoy, na kuondoa hofu ya kusuasua kwa uthabiti wa uchumi wa Umoja wa Ulaya.

Mvutano na Rajoy:

Sanchez alichaguliwa  kiongozi wa PSOE mwaka 2014, lakini alionndolewa baada ya uasi chamani mwake mwaka 2016 kwa kukataa kukiruhusu chama  cha Rajoy cha Popular Party (PP) kuunda serikali. Wakati huo, Sanchez alisema kuwa chama cha PP kilikuwa kinakumbwa na visa vingi vya ufisadi na hivyo hakingeongoza taifa. Alipata fursa ya kukiongoza tena chama chake cha  PSOE ambacho kilianzishwa miaka 140-iliyopita mwezi Mei mwaka 2017. Wakati PP kikikabiliwa na visa vya ufisadi, alimtaka Rajoy kujiuzulu na kuepuka kuwa waziri mkuu wa kwanza wa Uhispania kuondolewa madarakani kwa kura ya kutokuwa  na imani naye.

Pedro Sanchez Waziri Mkuu mtarajiwa
Pedro Sanchez Waziri Mkuu mtarajiwa Picha: Reuters/S. Perez

"Wakati wako umefika," Sanchez alisema. "Wewe ni sehemu ya historia, sura ambayo taifa linakaribia kuifunga." Rajoy alimjibu Sanchez kwa kusema kuwa alikuwa anajaribu kuunganisha serikali kutoka kwenye makundi mbali mbali ya kisiasa na kuwakumbusha wabunge kuwa Wasosholisti walikuwa wamepoteza uchaguzi mkuu mara mbili katika kipindi cha Sanchez.

Elimu na siasa:

Sanchez alijiunga kwa mara ya kwanza katika chama cha PSOE mwaka 1993 na kufanya kazi kama mshauri wa siasa katika Bunge la Ulaya na pia katika Umoja wa Mataifa wakati wa vita vya Kosovo. Alichaguliwa kuwa diwani katika Baraza la Mji wa Madrid mwaka 2004 na baadaye  akawa mjumbe wa Baraza  la wabunge la Uhispania akiuwakilisha mji wa Madrid mwaka 2009. Alishindwa uchaguzi wa  2011. Aliamua kukamilisha shahada yake ya uzamifu katika uchumi kabla ya kurejea bungeni mwaka 2013.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, dj, jm/rt (Reuters, AFP)

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman