Pele kusherehekea Krismasi hospitalini
22 Desemba 2022Hospitali anakotibiwa Pele, ya Albert Einstein ya mjini Sao Paolo, imesema Pele mwenye umri wa miaka 82 anahitaji uangalizi wa hali ya juu kutokana na kufeli kwa figo na moyo.
Hospitali hiyo imeripoti kuwa saratani ya Pele imezidi lakini hakuwa katika kitengo cha wagonjwa mahututi.
Pele anayezingatiwa na wengi kuwa mwanasoka bora wa wakati wote, alilazwa hospitali mjini Sao Paulo Novemba 29 kutoka na kile timu yake ya madaktari ilisema kutathmini tena matibabu yake ya mionzi, ambayo amekuwa akipatiwa tangu alipofanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe kwenye utumbo mwezi Septemba 2021.
Madaktari pia wamemgundua Pele, ambaye jina lake halisi ni Edson Arantes do Nascimento, na maambukizi kwenye mfumo wa kupumua.
Soma pia:Gwiji wa zamani wa Brazil Pele amtaka Putin kusitisha vita
Mapema mwezi huu, mabinti wa Pele, Kely Nascimento na Flavia Arantes walijaribu kuwahakikishia mashabiki kuhusu afya yake, wakikanusha ripoti kwamba Pele alikuwa amewekwa kwenye huduma za mwisho wa maisha, baada ya wafuasi hao kufanya mkesha nje ya hospitali.
Kely Nascimento, moja wa mabinti zake alisema watabaki na baba yako hospitali wakati wa Krismasi.
"Tuliamua pamoja na madaktari, kwa sababu nyingi, kwamba itakuwa vyema kwetu kubaki hapa" Kelly aliandika kwenye mtandao wake wa Instagram.
Wakisindikizwa na picha yao wakitabasamu, mabinti hao wa Pele waliwashukuru mashabiki wa baba yao kwa uungaji mkono na kuwatakia msimu mwema wa sikukuu, huku wakiahidi kutoa taarifa kuhusu maendeleo yake wiki ijayo.
Nyota ya Pele kwenye soka la dunia
Pele aling'aa tangu akiwa mdogo na kutwaa Kombe la Soka la Dunia mwaka 1958 akiwa na umri wa miaka 17.
Akifunga magoli matatu katika hatua ya nusu fainali na magoli mengine mawili katika fainali, na kuanza maisha yake ya soka na himaya ya soka ya timu ya taifa ya Brazil.
Pele alifunga zaidi ya mabao 1,000 katika moja ya maisha yenye simulizi nyingi zaidi za kimichezo.
Ndiye mchezaji pekee katika historia kuwahi kushinda makombe matatu ya dunia, mwaka 1958, 1962 na 1970.
Katika miaka ya karibuni, Pele, aliyepewa cheo cha mfalme, amekabiliwa na kuzorota kwa afya yakena ameonekana kwa nadra hadharani.
Soma pia:Kombe la Dunia: Brazil na Ureno zafuzu duru ya mtoano
Amepambana na hali yake kwa uchangamfu na ucheshi, na kuendeleza uwepo wake kwenye mitandao ya kijamii.
Pele alikuwa akichapisha mara kwa mara wakati wa mashindano ya Kombe la Dunia nchini Qatar, ikiwemo ujumbe wa pongezi kwa nahodha Lionel Messi baada ya Argentina kushinda kombe hilo.
Pele pia alitazama akiwa hospitali, wakati nyota wa Brazil Neymar, akifikia rekodi yake ya 77 na "Selecao."