Pengo baina ya matajiri na masikini ni kubwa Ujerumani
22 Desemba 2011
Hata mzozo wa madeni katika Umoja wa Ulaya ni mada inayoendelea kugonga vichwa vya habari. Basi tutaanza na gazeti la LANDESSZEITUNG linaloandika:
"Benki Kuu ya Umoja wa Ulaya, mara nyingine tena, imemimina takriban Euro nusu bilioni katika taasisi za fedha katika jitahada ya kuudhibiti mzozo wa madeni. Benki katika nchi za Ulaya, zimepatiwa mikopo yenye riba nafuu ya asilimia moja tu na zina muda wa miaka mitatu kuilipa mikopo hiyo. Kwa hivyo benki hizo sasa zinaweza kupumua angalao kwa kipindi hicho. Mabilioni yaliyotolewa na Benki Kuu ya Ulaya, hudhihirisha kuwa mzozo wa kiuchumi uliotikisa masoko ya fedha duniani miaka ya hivi karibuni, umetoa somo. Lakini ionekanavyo, baadhi ya wanasiasa huko Brussels, Berlin, Paris au London bado hawakutambua hilo."
Gazeti la HEILBRONNER STIMME likiandika kuhusu mada hiyo hiyo linasema:
" Baadhi ya wataalamu wanatumaini kuwa benki zilizopatiwa mikopo hiyo rahisi na Benki Kuu ya Ulaya, sasa zitanunua hisa zinazodhaminiwa na serikali za nchi zilizokumbwa na mzozo wa madeni na hivyo kuyasaidia mataifa hayo. Lakini hapo inafaa kuuliza; benki gani itanunua dhamana hizo, hali ukiwepo uwezekano mkubwa kuwa hatimae hazitokuwa na budi ila kuzisamehe fedha hizo. Vile vile, huo sio wajibu wa taasisi binafsi za fedha."
Tukiigeukia mada nyingine, gazeti la FLENSBURGER TAGEBLATT linaandika kuhusu umasikini unaozidi kuathiri familia nyingi hasa katika baadhi ya maeneo nchini Ujerumani:
"Bila shaka kuna sababu nzuri kwa serikali kutaka kupunguza umasikini na kupandisha kodi ya pato. Kwani uchunguzi wa maoni umeonyesha kuwa watu wanaoishi katika majimbo ambako kuna tofauti kubwa ya mapato, umma huo haukuridhika na serikali, kinyume na kule kwenye neema. Lakini jawabu sio kuongeza msaada wa fedha kwa wale wenye mapato ya chini au kuwapatia nafasi ya kusomea kazi mpya. Bora zaidi ni kwa serikali kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu na hiyo ni kuanzia shule za chekechea."
Sasa tukielekea Misri ambako mwanzoni mwa mwaka huu umma nchini humo sawa na wenzao katika ulimwengu wa Kiarabu, ulikuwa na matumaini mengi, gazeti la MÄRKISCHE ALLGEMEINE linaandika:
"Si matumaini yote yaliyotimika. Kinachotokea Misri hivi sasa kinaonyesha ukweli wa hali ya mambo. Hosni Mubarak ameondoshwa madarakani, lakini hiyo haimaanishi kuwa sasa kuna usawa wa haki kwa kila mmoja. Wanawake wanapaswa kuhofia hilo. Picha zilizonyesha jinsi mwanamke alivyonyanyaswa kwenye uwanja wa Tahrir umeughadhibisha ulimwengu mzima. Kitendo hicho kimedhihirisha kuwa hapo jeshi limevuka mpaka. Lakini kinachotia moyo ni kwamba wanawake wa Kimisri hawakubakia kimya. Wamesimama kidete na wameandamana kuupinga unyanyasaji huo. Hata hivyo, ukweli ni kwamba, bado kuna njia ndefu ya kwenda kabla ya kuwa na haki sawa nchini humo."
Mwandishi:MartinPrema/dpa
Mhariri:M.Abdul-Rahman