1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pillay alikosoa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

22 Agosti 2014

Mkuu wa Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Navi Pillay amelikosoa vikali Baraza la Usalama la umoja huo kwa kushindwa kuchukua hatua madhubuti za kumaliza au hata kuzuia mizozo inayoendelea.

https://p.dw.com/p/1Cz7J
Mkuu wa Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Navi Pillay
Mkuu wa Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Navi PillayPicha: Reuters

Akilihutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mjini New York jana Alhamisi kwa mara ya mwisho kabla ya kumaliza kipindi chake cha miaka sita, Agosti 30 mwaka huu, Bibi Pillay amesema baraza hilo limeshindwa kuchukua hatua madhubuti na mizozo inayoendelea kwa sasa ingeweza kuzuiwa na kwamba maamuzi ya pamoja ya baraza hilo, yangeweza kuokoa maisha ya watu.

Amesema maslahi binafsi ya kitaifa na tofauti za kisiasa zimesababisha baraza hilo kushindwa kufanya maamuzi ya pamoja. Pillay ametolea mfano mizozo inayoendelea nchini Syria, Iraq, Ukanda wa Gaza, Ukraine, Libya, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Sudan Kusini, Mali, Afghanistan, Somalia na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moonPicha: picture alliance / AA

Pillay amezitupia lawama nchi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akisema zimekuwa zikitumia kura zao za turufu kuzuia hatua zisichukuliwe katika kusitisha au hata kupunguza mizozo. Amesema hiyo siyo mbinu nzuri ya kujenga.

Pillay azitaka nchi wanachama kujizuia kutumia kura ya turufu

Amezitaka Marekani, China, Urusi, Ufaransa na Uingereza zijizuie kutumia haki yao kupiga kura ya turufu nyakati ambazo baraza hilo linachukua hatua ya kuzuia mizozo. Aidha, amelitaka baraza hilo kuzingatia dalili za mapema zinazojitokeza kama vile ukiukaji wa haki za binaadamu, likitilia maanani kwamba mizozo mingi inakuwa kwa miaka mingi.

Akilihutubia baraza hilo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon amemshukuru Bibi Pillay kwa utendaji wake wa kazi kipindi chote alipokuwa mkuu wa tume hiyo ya haki za binaadamu. Ban amesema anaamini wanachama wa baraza hilo watayafanyia kazi maoni ya Pillay pamoja na ripoti kuhusu ukiukaji mbaya wa haki za binaadamu unaoendelea duniani.

Mkuu mpya wa Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Mwanamfalme Zeid Ra'ad Zeid al-Hussein
Mkuu mpya wa Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa, Mwanamfalme Zeid Ra'ad Zeid al-HusseinPicha: picture-alliance/dpa

Katika mkutano huo wa jana, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipiga kura kwa kauli moja kupitisha azimio ambalo linaahidi kutumia mbinu makini zaidi kujaribu kuzuia vita katika siku zijazo.

Nafasi ya Navi Pillay itazibwa na Mwanamfalme wa Jordan Zeid Ra'ad Zeid al-Hussein, ambaye alikuwa balozi wa Jordan kwenye Umoja wa Mataifa. Zeid ataanza kazi rasmi Septemba Mosi mwaka huu.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,APE,RTRE
Mhariri:Josephat Charo