Ping akataa hukumu ya Mahakama ya Katiba Gabon
25 Septemba 2016Hatua hiyo ya Ping aliyoibainisha Jumamosi (24.09.2016) usiku inazusha uwezekano w kuibuka kwa mzozo mpya wa kisiasa katika nchi nhiyo ya Afrika ya kati inayozalisha mafuta.
Mahakama hiyo ilikubali ombi la Ping la kutaka kuangaliwa upya kwa matokeo ya uchaguzi huko Haut jimbo la Ogooue ambapo Bongo alitangazwa kuwa ameshinda kwa asilimia 95 kati ya asilimia 99.9 iliyojitokeza kupiga kura.
Hata hivyo katika hukumu hiyo iliyoitowa Ijumaa mahakama imegoma kupokea nakala za mahesabu ya kura yaliyotolewa na Ping kama ushahidi kwa madai kwamba alishindwa kuthibitisha udhati wake.
Wafuasi wa Ping watakiwa kuwa macho
Akizungumza na wafuasi wake na waandishi wa habari nyumbani kwake katika mji mkuu wa Barazavile Ping ametowa wito kwa wananchi kuwa macho na katika hali ya kujiandaa.
Ping ameongeza kusema "Tutahakikisha uamuzi wa wananchi unaheshimiwa.Mwaka 2016 hautokuwa sawa na ule wa mwaka 2009."
Ali Bongo ameingia madarakani katika uchaguzi tata wa mwamla 2009 kufuatia kifo cha baba yake Omar Bongo ambaye alikuwa rais wa Gabon kwa miaka 42. Ping mwanasiasa aliyekuwemo serikalini kwa muda mrefu nchini Gabon na pia kuwahi kutumika kama Mwenyekiti wa Halmashauri ya Afrika alikuwa mshirika wa karibu kwa Omar Bongo.
Rais Ali Bongo alijaribu kupunguza mvutano Jumamosi kwa kutowa wito wa kufanyika kwa mazungumzo na kuahidi serikali shirikishi.Ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters katika mahojiano kwamba "nasubiri kwa hamu kuwakaribisha wanachama wote wa vyama vyote vya kisiasa kuungana na juhudi zetu kwa kujiunga katika baraza la mawaziri."Amesema serikali mpya yumkini ikawajumuisha viongozi wakuu wa upinzani na hakufuta uwezekano wa kumtengea nafasi Ping.
Hata hivyo amekataa usuluhishi wa kimatatifa.Amesema "Hatuhitaji upatanishi wa kimataifa. Miongoni mwa Wagaboni tunafahamu namna ya mtun mmoja anayoweza kuzungumza na mwenzake."
Serikali chini ya shinikizo la kimataifa
Serikali ya Gabon ilikuwa ikiendelea kuwa chini ya shinikizo la kimataifa pale Jumamosi Umoja wa Ulaya ilipolalamika kwamba ujumbe wale waangalizi wa uchaguzi haukupewa nafasi kubwa katika kuangalia tathmini ya mahakama ya kuangalia upya matokeo.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini na Kamishna wa Maendeleo Nevn Mimica wamesema katika taarifa kutokana na hayo imani ya wananchi wa Gabon juu ya uhalali wa mchakato wa uchaguzi inaweza kutiliwa mashaka."
Wizara ya mambo ya nje ya mkoloni wa zamani wa nchi hiyo Ufaransa imeungana na kauli hiyo ya Umoja wa Ulaya kwa kusema katika taarifa kwamba uchunguzi wa mahakama juu ya matokeo haukuondowa mashaka yote.
Rais Idriss Derby wa Chad ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika ameupokea uamuzi huo wa mahakama na kumtaka Bongo kuweka mazingira yanayofaa ya kufanyika mazungumzo yatakayokuwa na tija.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters
Mhariri : Sudi Mnette