Pogba aipeleka Manchester United kileleni mwa Premier
13 Januari 2021Mashetani Wekundu kama wanavyojulikana kwa jina lao la utani, hawajawahi kuongoza jedwali tangu msimu wa mwaka 2012-13 wakati wa enzi za kocha mstaafu Sir Alex Ferguson.
United itasafiri hadi Anfield Jumapili ijayo kupambana na mabingwa watetezi Liverpool katika mechi ambayo inatajwa na wachambuzi wengi wa soka kuwa huenda ikaamua mustakabali wa ligi hiyo.
Ligi hiyo inaendelea tena leo usiku. Manchester City itakuwa nyumbani kuvaana na Brighton wakati Tottenham Hotspurs itakuwa na kibarua dhidi ya Fulham.
Na hapa Ujerumani, Bayern Munich inaingia uwanjani kuvaana na Hostein katika raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho la Ujerumani, DFB Pokal. Mechi hiyo itachezwa katika uwanja wa Holstein-Stadion.
Jana Jumanne Bayer Leverkusen ilipata ushindi muhimu dhidi ya Eintracht Frankfurt wa mabao 4-1. Ushindi wa Leverkusen umeiletea afueni kubwa timu hiyo baada ya kupoteza mechi zake za hivi karibuni za Bundesliga.
Nchini Uhispania, leo usiku kutashuhudiwa kivumbi kikali katika kombe la Super Cup wakati Real Sociedad itakapoikaribisha Barcelona katika uwanja wao wa nyumbani wa Estadio Nuevo Arcangel.
Mechi hiyo ni nusu fainali inatokea siku moja tu baada ya Athletico Madrid kuinyuka Sevilla mabao 2-0 na kuhakikisha inasalia juu ya jedwali la Ligi Kuu ya Uhispania La Liga.
Athletico ina alama 41 ikifuatiwa na Real Madrid katika nafasi ya pili yenye alama 37, Barcelona ni ya tatu ikiwa na alama 34.
Chanzo: Mashirika