Poland yaadhimisha miaka 80 tangu Uasi wa Warsaw
1 Agosti 2024Agosti Mosi, 1944, wanajeshi hao wakiongozwa na Jeshi la Kitaifa walipambana na vikosi vya NAZI kwa lengo la kuikomboa Warsaw dhidi ya uvamizi wa Wajerumani.
Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier aliyehudhuria hafla hiyo, ameomba radhi kwa madhila waliyopitia Wapoland mikononi mwa watawala wa kinazi wa Ujerumani. "Frank-Walter Steinmeier: Ndugu wastaafu, kila neno litakuwa ni dhaifu sana kuelezea unyama huu. Ndio maana nataka kusema sentensi moja tu. Inatoka moja kwa moja kutoka moyoni: Ninaomba msamaha. Utaifa, ubeberu na ubaguzi wa rangi ulisababisha ukatili ambao Wapoland walilazimika kujitetea kwa Uasi wa Warsaw. Hili halipaswi kutokea tena."
Ingawa uasi huo ulishindwa, lakini Rais wa Poland Andrzej Duda ameutaja kama "msingi wa maadili ya uhuru wa Poland" wakati wa hafla ya kumbukumbu hiyo jana Jumatano.