1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Poland yaufananisha mzozo wa wahamiaji na vita baridi

22 Novemba 2021

Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki ameutaja mzozo wa uhamiaji kwenye mpaka wa nchi yake na Belarus, kama jaribio kubwa la kuiyumbisha Ulaya tangu enzi za vita baridi.

https://p.dw.com/p/43Jmz
EU-Parlament | Polen Ministerpräsident Mateusz Morawiecki
Picha: Ronald Wittek/AP/picture alliance

Kiongozi huyo wa Poland pia ametahadharisha juu ya uwezekano wa wimbi jipya la wahamiaji kutoka Afghanistan na Uzbekistan watakaojaribu kuingia ndani ya mataifa ya Umoja wa Ulaya. 

Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki ameyasema hayo wakati akijitayarisha kukutana na viongozi wa Umoja wa Ulaya katika wakati ambapo Poland inakabiliwa sio tu na mzozo wa wahamiaji bali pia mvutano kati yake na Brussels kutokana na madai kuwa inakiuka ahadi zake za kuheshimu sheria za Umoja huo.

Soma pia: Lukashenko kufanya mazungumzo na Merkel juu ya uhamiaji

Morawiecki amesema Poland haitobadilisha msimamo wake na kwamba itafanya kila iwezavyo kulinda mipaka ya Umoja wa Ulaya. Ametahadharisha kuwa, hali hiyo ya mzozo wa wakimbizi inayoikumba Poland pia inaweza kuzikumba Ujerumani, Ubelgiji, Ufaransa na Uhispania.

Waziri Mkuu huyo ameandika kwenye mtandao wake wa Twitter kuwa Rais wa Belarus Alexander Lukashenko ameanzisha vita dhidi ya Umoja wa Ulaya na kuwa ni jaribio la kuiyumbisha Ulaya.

"Huu ni mwanzo tu wa mgogoro mrefu ambao umepangwa na utawala wa Lukashenko, labda kwa ushirikiano na Ikulu ya Kremlin. Katika miezi ya hivi karibuni, Belarus imezidisha harakati zake, kwa hivyo ni muhimu kueleza kwamba huu sio mzozo na Poland au Lithuania lakini ni jaribio la kukiuka mipaka ya NATO na Umoja wa Ulaya."

Poland inadai Lukashenko anapata uungwaji mkono wa Rais wa Urusi

Deutschland Bundeskanzlerin Merkel in Warschau
Kansela Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Poland Mateusz MorawieckiPicha: Czarek Sokolowski/AP/dpa/picture alliance

Morawiecki pia amedai kuwa Lukashenko anapata uungwaji mkono wa Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Mataifa ya Magharibi yameishtumu Belarus kwa kuanzisha mgogoro huo kimakusudi kwa kuwachukua wahamiaji -wengi wao kutoka Mashariki ya Kati na kuwapeleka kwenye mpaka wa Poland na kuwaahidi kuwavusha ndani ya Umoja wa Ulaya.

Belarus imekanusha madai hayo na badala yake kuibebesha lawama Umoja wa Ulaya kwa kukosa kuwapa hifadhi wahamiaji hao.

Hata hivyo katika hatua ya kushangaza, Lukashenko ameliambia shirika la habari la Uingereza la BBC kuwa upo uwezekano vikosi vyake vya usalama vilisaidia watu kuvuka mpaka na kuingia Umoja wa Ulaya, japo amekanusha kuhusika.

Soma pia: UN kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu Belarus

Morawiecki amesema atazitembelea nchi za Umoja wa Ulaya wiki hii ili kuwahimiza viongozi wa nchi hizo kutoruhusu matatizo yanayojadiliwa kati ya Poland na Brussels kuchukua nafasi kubwa zaidi na kulifumbia macho suala la wakati huu juu ya mzozo wa wahamiaji.

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wanasema Poland inatumia suala la mzozo wa wahamiaji ili kuzima mjadala juu ya mageuzi katika mfumo wake wa mahakama, mageuzi ambayo Umoja wa Ulaya unaamini kuwa unaingilia uhuru wa mahakama.

Jana Jumapili, walinzi wa mpakani wa Poland waliwazuia takriban wahamiaji 100 waliokuwa wakijaribu kwa nguvu kuingia nchini humo. Kwa mujibu wa kura ya maoni iliyochapishwa na gazeti la kila siku la Rzeczpospolita, zaidi ya asilimia 55 ya Wapoland wana wasiwasi kwamba mgogoro huo wa wakimbizi huenda ukageuka na kukasababisha vita.

Wakati hayo yanaripotiwa, mkimbizi raia wa Yemen alizikwa katika kijiji cha Bohoniki. Wizara ya mambo ya nje ya Yemen imesema mwanamume huyo alikufa kutokana na baridi kali.