1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAustralia

Polisi Australia yachunguza chanzo cha shambulizi la Sydney

15 Aprili 2024

Polisi nchini Australia wamesema wanachunguza ni kwa nini mtu wa umri wa miaka 40 aliye na matatizo ya akili alionekana kuwalenga wanawake wakati wa shambulizi la kisu kwenye jumba la maduka mjini Sydney.

https://p.dw.com/p/4ekp1
Shambulizi la kisu Sydney
Polisi wanasema muuwaji aliwalenga wanawake katika shambulizi hilo la Jumba la maduka la WestfieldPicha: Steven Saphore/AP Photo/picture alliance

Polisi nchini Australia wamesema leo kuwa wanachunguza ni kwa nini mtu wa umri wa miaka 40 aliye na matatizo ya akili alionekana kuwalenga wanawake wakati alipokuwa akizurura kwenye jumba la maduka mjini Sydney akiwa na kisu kikubwa, na kuwauwa watu sita na kuwajeruhi wengine kadhaa.

Video zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zilimuonesha Joel Cauchi akiwawinda waathiriwa wa kike wakati akizurura kwenye jumba la maduka la Westfiled lilokuwa limejaa watu Jumamosi mchana.

Watano kati ya waathiriwa sita waliouawa walikuwa wanawake, pamoja na waliojeruhiwa. Kamishna wa polisi wa New South Wales Karen Webb amesema video hizo zinaonyesha kuwa mshukiwa huyo aliwalenga wanawake. Shambulizi hilo la Cauchi, ambalo lilidumu kwa karibu nusu saa, lilihitimishwa wakati inspekta wa polisi Bi Amy Scott alipompiga risasi na kumuuwa. Waziri Mkuu wa Australia Anthony Albanese amesema amezungumza na familia za baadhi ya waathiriwa.