1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi imetoa taarifa walipo viongozi wa Chadema

22 Julai 2021

Jeshi la polisi mkoani Mwanza limetoa taarifa kuhusu walipo viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, Chadema akiwemo Mwenyekiti wa taifa Freeman Mbowe.

https://p.dw.com/p/3xpiD
Tansania Opposition Freeman Mbowe
Picha: Ericky Boniphace/AFP/Getty Images

Taarifa hiyo imetolewa leo baada ya kuwepo mjadala mkubwa kutaka kujua sehemu waliko viongozi hao waliokamatwa saa chache kabla ya kufanyika kwa kongamano la kudai Katiba Mpya lililokuwa limeandaliwa na Baraza la Vijana la chama hicho, Bavicha.

Kamanda wa Polisi mkoani Mwanza Ramadhani Ng'anzi amesema Mbowe, na mwenyekiti wa Baraza la Vijana taifa John Pambalu pamoja na wanachama wengine 14 waliokamatwa wanashikiliwa na jeshi la polisi. Soma Chadema yawaamuru wafuasi wake kumsaka Mbowe

Kamanda Ng'anzi amesema Mbowe anashikiliwa katika kituo cha makao makuu ya jeshi la polisi jijini Dar es Salaam, huku wanachama wengine wakiwa wanashikiliwa katika kituo kikuu cha polisi mkoni Mwanza. 

Katazo la Kongamano

Tansania Wahlen | Treffen der Chadema-Delegierten in Dar es Salaam
Picha: DW/S. Khamis

Katazo la kongamano kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel alilolitoa siku moja kabla na hili la leo kutoka kwa kamanda wa polisi linadai Mwanza kuna maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19, hivyo mikusanyiko isiyo ya lazima hairuhusiwi. Hata hivyo, waandishi wa habari wanauliza ni mazingira gani yalizuia kongamano la Chadema lililotarajia kuwa na washiriki 300 na kuruhusu mkusanyiko wa watu zaidi ya elfu tano katika Uwanja wa Nyamagana kushuhudia mchezo wa kandanda kati ya Pamba ya Mwanza na Coast Union ya Tanga. soma Chadema kuendelea na makongamano ya Katiba mpya

Kuzuiwa kwa kogamano la Chama kikuu cha upinzani Chadema na kuwekwa ndani kwa baadhi ya viongozi na wanachama hao kunatokea siku chache tangu Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kuwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa vyama vya siasa vinaweza kuendelea na mikutano ya ndani huku vikisubiri utaratibu mwingine wa miktano ya nje.