Maafisa wa chama cha Imran Khan washikiliwa na polisi
10 Septemba 2024Wabunge kadhaa na viongozi wa chama cha waziri mkuu wa zamani wa Pakistan Imran Khan, wanashikiliwa na polisi katika msako uliofanyika siku moja baada ya mkutano mkubwa wa chama hicho kushinikiza kuachiliwa kwa Khan.
Nyota huyo wa zamani wa mchezo wa kriketi mwenye umri wa miaka 71, amekuwa gerezani kwa zaidi ya mwaka mmoja tangu kuondolewa kwake madarakani mwaka 2022, baada ya kutofautiana na majenerali wa kijeshi wa Pakistan, ambao mara nyingi wanaamua nani atatawala taifa hilo lenye wakaazi milioni 241.
Polisi imesema imewakamata watu wanne ingawa chama kinadai kuwa wanachama 13 wamekamatwa katika maeneo tofauti mjini Islamabad, ikiwemo nje ya majengo ya bunge.
Wagombea wanaoungwa mkono na chama cha Khan cha Pakistan Tehreek-e-Insaf PTI, walishinda viti vingi zaidi katika uchaguzi wa Februari lakini hawakuwa na idadi kubwa kuunda serikali.