Polisi yatishia kuwapiga waandamanaji kama "mbwa koko"
26 Aprili 2018Maandamano hayo yaliyopigwa marufuku - ambayo yalipangwa kufanyika Alhamisi katika siku ya maadhimisho ya muungano kati Tanganyika na Zanzibar, yaliitishwa na mwanaharakati aliejipeleka uhamishoni nchini Marekani Mange Kimambi.
"Wanaopanga kuandamana kesho watakiona cha moto, watapigwa kama mbwa koko." Alisema Gilles Muroto kamanda wa jeshi la polisi wa mji mkuu wa utawala wa Dodoma wakati akiongea na waandishi wa habari siku ya Jumatano.
Hofu ya kurudi Tanzania
Katika mji wa kaskazini mwa Tanzania wa Arusha, ambao ni ngome ya upinzani polisi iliwakamata Jumanne watu saba ikiwatuhumu kwa kuwahamasisha Watanzania kushiriki katika maandamano hayo yaliopigwa marufuku.
Mange Kimambi anayeishi Los Angeles nchini Marekani, anawafuasi milioni 1.8 katika mtandao wa kijamii wa Instagram ambako anajipambanua kama mwanaharakati wa demokrasia, Mtanzania mwenye fahari."
Anasema kuwa anaogopa kurudi Tanzania kwa kuhofia kunyanyaswa na serikali kwa sababu ya kuwakosoa viongozi wenye mamlaka. Picha za kwenye televisheni zinaonesha askari polisi walio na silaha wakiwa katika miji kadhaa mikubwa ya Tanzania na kuwonya wanachi wasishiriki maandamano ambayo yamepigwa marufuku na serikali.
Hofu ya kuutia doa utawala wa Magufuli
Maandamano nchi Tanzania hata kwa kiwango kidogo, yanatazamiwa kutia dosari kwa uongozi wa Rais John Pombe Magufuli anaedaiwa kuua upinzani na uhuru wa kujieleza tangu alipoingia madarakani rasmi mwaka 2015.
Magufuli alionya juma lililopita kuwa mtu yeyote anayepanga kuandamana, atakutana na mkono wa sheria na kusema kuwa kamwe serikali yake haitaruhusu mageuzi ya kiuchumi yaliofanyika kuharibiwa na waandamanaji wachache wasiotii sheria.
Ushawishi wa Mange Kimambi
Lakini Kimambi alisisitiza katika mitandao ya kijamii kuhusu watu kuandamana Aprili 26, kushinikiza Magufuli aachie madaraka. Maandamano kama haya yaliwahi kuitisha tena na chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania Chadema mwaka 2016 lakini hayakufanikiwa kutokana na upinzani kutoka kwa serikali iliyopo madarakani.
Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulitoa tahadhari juu ya uwezekano wa kutokea vurugu kwa waandamanaji. Maria Sarungi Tsehai aliebobea katika masuala ya mawasiliano na mtu maarufu nchini Tanzania, mwezi huu aliandika katika blogu kuwa "Nguvu kubwa inayotumiwa na serikali kuzuia maandamano, inatosha kuonesha ushawishi alionao Mange Kimambi kwa vijana".
Aidha iliongeza kuwa, "kama mwanamke aliepo Los Agelea anaweza kuhamasisha watanzania kudai haki zao kupitia maandamano na kuitaka serikali iwajibike na viongozi wakubwa wa serikali wanatoa vitisho kuhusu hayo maandamano hiyo inadhihirisha kwamba athari za Mange Kimambi kwa serikali ni kubwa." Aliandika Tsehai.
Mwandishi: Veronica Natalis/ Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga