1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi ya Misri yawatawanya waandamanaji

Admin.WagnerD14 Agosti 2013

Vyombo vya usalama nchini Misri vimeanzisha operesheni kubwa kuwatawanya wafuasi wa rais aliyepinduliwa, Mohamed Mursi kutoka kambi mbili kubwa mjini Cairo. Watu zaidi ya 43 wameuawa katika ghasia zilizofuata.

https://p.dw.com/p/19P8v
Cairo yawaka moto
Cairo yawaka motoPicha: picture-alliance/dpa

Operesheni hiyo imeanza muda mfupi baada ya mapambazuko alfajiri ya leo. Maafisa wa usalama walizizingira kambi za Rabaa al-Adawiya na al-Nahda, ambazo ziko katika maeneo tofauti ya mji mkuu Cairo, wakisindikizwa na tingatinga.

Watu waliokuwepo wameliambia shirika la habari la AFP kuwa wanajeshi walitumia magari maalum kuwamwagia waandamanaji maji ya kuwasha, na vile vile walirusha mabomu ya kutoa machozi. Kwa mujibu wa mashahidi hao, mashambulizi hayo yaliwaweka waandamanaji katika hali ya mkanyagano.

Katika upande mmoja wa kambi, yalikuwepo makabiliano baina ya waandamanaji na maafisa wa usalama, ambayo yalifuatiwa na milio ya risasi, ambazo imethibitika zilifyatuliwa na polisi.

Picha za televisheni zimeonyesha watu waliojeruhiwa wakiwa wanakimbizwa katika vituo vya dharura vya matibabu, na polisi waliokuwa wakiwaburura waandamanaji waliokaidi kuondoka.

Polisi imeshutumiwa kutumia nguvu kupindukia kupambana na waandamanaji
Polisi imeshutumiwa kutumia nguvu kupindukia kupambana na waandamanajiPicha: KHALED DESOUKI/AFP/Getty Images

Nguvu kupita kiasi

Waandamanaji wameilaumu polisi kutumia nguvu kubwa kupita kiasi, katika kuwatawanya.

''Mashambulizi yalikuwa ya ghasia kubwa. Polisi imetumia mabomu ya kutoa machozi, risasi za moto na za mpira, na aina zote za ukandamizaji kujaribu kuwatimua waandamanaji. Watu wamepoteza maisha yao.'' Alisema mmoja wa waandamanaji.

Kwa mujibu wa tangazo la wizara ya ndani ya Misri, tayari polisi imeweza kuwaondoa kabisa waandamanaji kutoka kambi ndogo ya katika viwanja vya al-Nahda. Vile vile afisa mmoja wa usalama ameiambia AFP kuwa watu kadhaa wanaomuunga mkono Mursi wamekamatwa kwa msaada wa wakazi wa maeneo jirani.

Miongoni mwa hao waliokamatwa wameonekana wakiwa wamechuchumaa chini, wakizingirwa na maafisa wa usalama.

Aidha, vituo vya televisheni vimeonyesha familia za watu waliokuwa wamekita kambi katika uwanja wa al-Nahda, miongoni mwao wakiwemo watoto na wanawake, wakiwa wanauhama uwanja huo, wakisindikizwa na polisi.

Udugu wa kiislamu wakaza kamba

Huku hayo yakijiri, kundi la udugu wa kiislamu la Mohamed Mursi limewataka wafuasi zaidi kujimwaga mitaani, kulaani kile wanachokiita ''mauaji ya halaiki''. Msemaji wa kundi hilo Gehad al-Haddad amesema kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, kuwa kinachoendelea sio juhudi za kuwatawanya waandamanaji, bali jaribio la kunyamazisha sauti ya upinzani dhidi ya mapinduzi ya kijeshi.

Hakuna dalili kuwa wafuasi wa Mursi wanasalimu amri
Hakuna dalili kuwa wafuasi wa Mursi wanasalimu amriPicha: picture-alliance/dpa

Msemaji huyo hali kadhalika alisema kuwa watu 250 wamekwishauawa, na wengine zaidi ya 500 wamejeruhiwa.

Mwandishi wa shirika la habari la AFP amesema amehesabu maiti 43 kwenye kituo cha muda cha kuhifadhia maiti katika eneo la Rabaa al-Adawiya, na kuongeza kuwa wengi wa marehemu walionekana kuuawa kwa risasi. Mwandishi huyo amesema hakuona maiti za watoto, wala za wanawake.

Viongozi wa waandamanaji watiwa mbaroni

Wizara ya mambo ya ndani ya Misri, imesema kuwa maafisa wawili wa polisi pia wameuawa. Wizara hiyo pia imearifu kuwa viongozi kadhaa wa udugu wa kiislamu wametiwa mbaroni, lakini hawakutaja majina yao.

Taarifa za hivi karibuni zinaeleza kuwa waandamanaji wanaomuunga mkono Mohamed Mursi wameshambuliana na vikosi vya usalama katika miji ya Minya na Assiut, ambako kanisa la madhehebu ya Koptiki limechomwa moto.

Hatua hii ya serikali ya mpito kuingilia kati kuwatawanya waandamanaji imechukuliwa saa chache baada ya Marekani kuitolea wito kujizuia kufanya hivyo, na kuitaka kuwaruhusu wapinzani kuandamana kwa uhuru. Umoja wa Ulaya umeitaka serikali mjini Cairo kujizuia.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFPE/RTRE/APE
Mhariri: Josephat Charo