Polisi ya Ujerumani yajiweka tayari kwa maandamano Chemnitz
30 Agosti 2018Hali hiyo imezuka kutokana na shambulio la kuchomwa kisu mtu mmoja na kufariki limezusha ghasia za makundi ya kibaguzi. Polisi ya jimbo la Saxony imesema itapata msaada wa polisi zaidi kutoka majimbo mengine matano pamoja na polisi kutoka serikali kuu ya shirikisho, baada ya kuzidiwa idadi kwa kiasi kikubwa na maelfu ya wanazi, mamboleo, wahuni katika michezo na watu wengine wenye misimamo mikali katika ghasia za siku ya Jumapili na Jumatatu.
Mji wenye matatizo wa Chemnitz , ambako waziri mkuu wa jimbo hilo Michael Kretschmer alikuwa afanye mkutano utakaojadili demokrasi, umeshuhudia kuzuka kwa ghasia zilizokuwa zikitokota kwa muda mrefu kutokana na ghadhabu zilizosababishwa na kile waandamanaji wanachosema kuwa ni "uhalifu wa wahamiaji" tangu pale alipouwawa mtu mmoja kwa kuchomwa kisu siku ya Jumapili.
Polisi wamewakamata Yousif Ibrahim A, kutoka Iraq mwenye umri wa miaka 22, na Alaa S. kutoka Syria mwenye umri wa miaka 23, kwa kumchoma kisu Daniel H. fundi seremala mwenye umri wa miaka 35, uhalifu ambao ulizusha mashambulizi mitaani dhidi ya watu ambao magenge hayo yaliwaona kuwa ni wageni.
Matukio hayo ya kuchukiza, ambayo yalishuhudia mashambulizi dhidi ya mtu mmoja kutoka Afghanistan, Syria na Bulgaria na yamezusha hali ya mabadiliko ya mawazo ndani na nje ya Ujerumani.
Ashambuliwa kwa minyororo ya chuma
Katika uhalifu mwingine uliosababishwa na chuki usiku katika eneo la mashariki la iliyokuwa Ujerumani ya kikomunist , mhamiaji mwenye umri wa miaka 20 alishambuliwa kwa matusi ya chuki dhidi ya wageni, alipigwa mateke na kupigwa na minyororo wa chuma na watu watatu katika mji wa pwani ya habari ya baltic wa Wismar, polisi imesema bila kueleza anatoka nchi gani.
Picha za waandamanaji wakitoa salaam iliyopigwa marufuku ya enzi za utawala wa Hitler katika maandamano ya siku ya Jumatatu , zilikuwa zinashitua, " alisema mkuu wa haki za binadmu wa Umoja wa mataifa Zeid Ra'ad Al-Hussein , akiwataka wanasiasa kutoka mataifa yote ya Ulaya kukemea hali hiyo.
Kansela Angela Merkel ambaye yuko katika ziara ya mataifa ya Afrika hadi Ijumaa, kwa kiasi kikubwa kujadili jinsi ya kupambana na sababu za uhamiaji kwenda Ulaya, ameshutumu maandamano hayo ya wenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia, akisema hakuna nafasi kwa "chuki katika mitaa" katika taifa hilo la demokrasia ya kiliberali.
Uhalifu unaofanywa na wahamiaji mara nyingi huchukuliwa na waungaji mkono wa chama cha mrengo mkali wa kulia cha Alternative for Germany, chama mbadala kwa Ujerumani AfD, pamoja na vuguvugu la maandamano ya mitaani la Wazalendo wa Ulaya wanaopinga Uislamu, PEGIDA , ambao wanamuona Merkel kama msaliti kwa kuruhusu wahamiaji kuingia nchini humo.
Mwandishi: Sekione Kitojo/afpe
Mhariri: Mohamed Khelef