1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pompeo azuru China

Shisia Wasilwa
14 Juni 2018

Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Marekani amekutana na rais wa China Xi Jinping na waziri wa mambo ya kigeni wa taifa hilo Wanng Yi Alhamisi (14.06.2018).

https://p.dw.com/p/2zau6
Südkorea Mike Pompeo und Taro Kono
Picha: Reuters/Kim Hong-ji

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo amekutana na viongozi wa serikali ya China kuhusu suala la Korea Kaskazini. Pompeo amemwambia rais wa China Xi Xinping wakati wa mkutano wao mjini Beijing kwamba Marekani inataka amani ya kudumu na thabiti katik eneo hilo.

Pompeo aliwasili Beijing akitokea mjini Seoul Korea Kusini ambako alisema Marekani imejitolea kuhakikisha kuwa mpango wa kuondoa silaha za nyukilia Korea Kaskazini "umethibitishwa na umekamilishwa," baada ya mkutano wa kihistoria uliofanyika nchini Singapore kati ya marais wa mataifa hayo mawili. Hata hivyo wakosoaji wamesema kuwa mpango huo haukuwa na utaratibu wa jinsi Korea Kaskazini itakavyoondoa silaha hizo za nyuklia.

 "Tunaamini kuwa Kim Jong Un anafahamu dharura iliyopo...kwamba tunastahili kutimiza hili haraka," Pompeo alisema kuhusu jitihada za Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa silaha za nyuklia.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani alizuru mjini Seoul kumfahamisha mwanadiplomasia mwengine wa Japan baada ya matamshi ya rais Donald Trump kuibua sintofahamu na wasiwasi jijini Tokyo na Seoul.

Pompeo azungumzia kuondolewa silaha za nyuklia

Lakini kwenye mkutano wa pamoja na mawaziri wa masuala ya kigeni wa mataifa hayo mawili, Pompeo amesisitiza kuwa hakuna mwangaza kuhusu jinsi ya kufikia mpango wa kuondoa silaha za nyuklia Korea Kaskazini.

Donald Trump und Kim Jong Un Singapur
Kim Jong Un, kushoto, na Donald Trump, walipokutana Singapore 12.06.2018Picha: Reuters/K. Lim

Kauli ya Pompeo inajiri wakati vyombo vya habari vya kitaifa vya Korea Kaskazini vikiripoti kuwa Trump hakuwa tu ametoa pendekezo la kusitisha mazoezi ya jeshi la Marekani kwenye mazungumzo hayo lakini pia kuondoa vikwazo dhidi ya Pyongyang.

Trump alisema hayo baada ya kukutana na Kim -- mkutano wa kwanza kati ya viongozi waliopo mamlakani wa Marekani na Korea Kaskazini--kwamba Marekani itasitisha mazoezi yake ya pamoja na jeshi la Korea Kusini, kauli ambayo imezishangaza Korea Kusini na Marekani.

Licha ya wasiwasi miongoni mwa washirika wa karibu wa Marekani na wadadisi, utawala wa Trump unaendelea kusisitiza kuwa mkutano wa rais Trump na Kim ulikuwa wenye mafanikio makubwa.

Mwandishi: Shisia Wasilwa/afp, dpa

Mhariri: Josephat Charo