Pope yuko Istanbul
29 Novemba 2014Papa Francis atagusia masuala kadhaa ya urithi mkubwa wa mji huo mkubwa wa Uturuki, ambao kama Constantinople ulikuwa mji mkuu wa enzi ya Wakristo wa Byzantine hadi pale Ottoman ambaye alikuwa Muislamu alipouteka mji huo mwaka 1453.
Ataanza ziara yake kwa kutembelea Hagia Sophia , kanisa kuu la enzi za Byzantine ambalo lilibadilishwa kuwa msikiti baada ya kutekwa kwa mji wa Constantinople lakini baadaye likawa jengo la makumbusho kwa watu wa imani zote katika Uturuki ya enzi za mpya.
Jicho la Uchunguzi
Kila atakalofanya litaangaliwa kwa jicho la uchunguzi baadaye leo wakati akifanya ziara katika msikiti wa Sultan Ahmet , unaofahamika kama msikiti wa buluu, moja kati ya usanifu mkubwa wa majengo katika enzi za utawala wa Ottoman.
Wakati mtangulizi wake Benedict 16 alipozuru msikiti huo mwaka 2006, alifuata utaratibu wa sala ya Kiislamu na kuelekeza uso Mecca katika kile wengi walichokiona kuwa ni ishara ya kushangaza ya maridhiano.
Vatican baadaye iliweka wazi kwamba hakuwa akisali katika msikiti huo lakini alikuwa "katika taamuli".
Papa Francis huenda akafanya kama hivyo.
Baadaye mchana leo kiongozi huyo wa kanisa Katoliki ataongoza sala katika kanisa Katoliki la Roho Mtakatifu mjini Istanbul.
Mtaguso wa Kanisa
Baadaye atafanya sala ya mtaguso wa kanisa , au tapo la kuleta umoja miongoni mwa imani za Kikristo katika kanisa la Orthodox la Mtakatifu George pamoja na mkutano wa faragha na askofu mkuu Bartholomew 1, mkutano wa kwanza katika kiwango cha usawa , kwa waumini wanaokadiriwa kufikia milioni 300 wa kanisa la Orthodox duniani.
Francis na Bartholomew, ambao wana uhusiano mzuri -- watajaribu kupunguza tofauti zao baina ya makanisa hayo mawili ambazo zimekuwapo tangu enzi za mtengano mkuu katika mwaka 1054.
"Tunasubiri kwa hamu ziara ya ndugu yetu, Papa Francis, "Bartholomew amesema kabla ya ziara hiyo. "Itakuwa hatua nyingine muhimu katika uhusiano wetu kama makanisa ndugu."
Jamii ya waumini wa Kikristo nchini Uturuki ni ndogo, kiasi ya watu 80,000 katika nchi yenye kiasi ya Waislamu 75 milioni -- lakini pia ikiwa ina mchanganyiko mkubwa , ikiwa na Warmenia , Wagiriki ambao ni waumini wa kanisa la Orthodox, Wafaransa Walevantini, Wasyria Waorthodox na Wachaldeani.
Miongoni mwa hao wote ni Wafaransa-walevantini na jamii ya Wachaldeani ndio wanaomtambua Papa kama kiongozi wa kanisa lao.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Amina Abubakar