1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

POSTDAM: Marekani na Russia zazozania kituo cha kukinga makombora Ulaya.

31 Mei 2007
https://p.dw.com/p/CBwH

Marekani na Russia zimekuwa na mvutano kuhusu mpango wa Marekani wa kujenga kituo cha kukinga makombora barani Ulaya.

Waziri wa mambo ya nje wa Russia, Sergei Lavrov na mwenzake wa Marekani, Bibi Condoleezza Rice wamejibizana vikali kuhusu mpango wa Marekani wa kujenga kituo hicho katika eneo la Ulaya Mashariki.

Hapo awali Bibi Codoleezza Rice alikuwa amesema kwamba madai ya Russia hayana msingi wowote.

Mataifa hayo pia yalitofautiana kuhusu hatma ya jimbo la Kosovo ambapo Marekani inapendekeza jimbo hilo liwe huru kutoka Serbia lakini liwe na usimamizi wa kimataifa, huku Russia ikipinga pendekezo hilo.

Mawaziri hao walikuwa katika mji wa Postdam, Ujerumani, kwenye kikao cha maandilizi ya mkutano wa wiki ijayo wa wakuu wa mataifa manane yaliyostawi kiviwanda, G8.

HEILEGENDAM

Maafisa wa usalama wa Ujerumani wameuzingira mji wa kitalii wa Heilegendamm kabla ya mkutano wa juma lijalo wa mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa manane yaliyostawi kiviwanda, G8.

Ua mrefu wa seng´enge wa kiasi kilomita kumi na mbili umejengwa kuuzunguka mji huo ili kuwazuia waandamanaji kuwatatiza viongozi wa kimataifa wanaotarajiwa kuhudhuria mkutano huo.

Maafisa wanasema askari wa usalama kiasi elfu kumi na sita wamepelekwa katika eneo hilo kukabiliana na watu laki moja wanaotarajiwa kujitokeza kuupinga mkutano huo.

BERLIN

Wapatanishi wa kimataifa wa mzozo wa Mashariki ya Kati wamesema wanapanga kukutana na Israil pamoja na Wapalestina mwezi ujao kujaribu kuanzisha mazungumzo ya ana kwa ana ya kutafuta amani katika eneo hilo.

Akizungumza mjini Berlin baada ya mkutano wa kundi la pande nne linaloshughulikia amani ya Mashariki ya Kati, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, amesisitiza haja ya kukomesha mashambulió na ulipizaji kisasi katika eneo hilo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Bi Condoleezza Rice, amesema:

O TON RICE

" Ninaamini kundi la pande nne limeshughulikia zaidi suala hili katika kipindi cha miezi sita iliyopita pengine kuliko kipindi kingine chochote ambacho nimekuwa waziri wa mambo ya nje.

Kuhusu mahakama ya kimataifa ya mauaji ya Hariri, hilo si suala la kuingilia mambo ya ndani ya Lebanon. Vinginevyo ni hatua ya kuulinda uhuru wa nchi hiyo"

Kundi hilo linalojumuisha Umoja wa Ulaya, Russia, Umoja wa Mataifa na Marekani, limetoa taarifa inayowashutumu wanamgambo wa Kipalestina kwa kuvurumisha makombora kusini mwa Israil.

Taarifa hiyo pia imeitaka Israil kuzingatia kwa makini inapoendesha harakati zake za kiusalama ili ipunguze idadi ya raia wanaojeruhiwa katika makabiliano hayo.

Kundi hilo pia limetoa wito Israil iwaachie huru viongozi wa Hamas inaowashikilia.