PRAGUE:Bush katika mazungumzo na wakuu wa Czech
5 Juni 2007Rais George Bush wa Marekani amewasili katika mji mkuu wa Jamuhuri ya Czech Prague ikiwa ni kituo chake cha kwanza katika ziara ya siku nane barani Ulaya.
Ziara hiyo ya Rais Bush ina nia ya kuupigia upatu zaidi mpango wake wa kuweka makombora ya kujihami Ulaya ya Mashariki.Marekani imepanga kuweka makombora hayo Poland na Czech katika kile inachodai kujilinda na mashambulizi ya Iran na Korea Kaskazini.
Rasi Bush amepanga kukutana na wakuu wa Czech, Rais Vaclav Klaus na Waziri Mkuu Mirek Topolanek ambao wanauunga mkono mpango huo.
Hata hivyo mpango huo unapingwa vikali na Urusi, ambapo rais Vladmir Putin wa nchi hiyo ametishia kuelekeza makombora yake Ulaya iwapo Marekani itaendelea na mpango wake huo.
Rais Putin na Rais Bush wanatarajiwa kuwa na mazungumzo pembezoni mwa mkutano wa wakuu wa nchi za G8 mjini Hailengdamm Ujerumani.