1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Primier yaitia kiwewe Bundesliga usajili

26 Juni 2015

Hofu ya vilabu vya ligi kuu ya Uingereza Premier League kumwaga fedha kuwasajili wachezaji wa ligi kuu ya Ujerumani-Bundesliga imetawala, lakini wengine wanasema Bundesliga inaweza kufaidika kutokana na pato la ziada.

https://p.dw.com/p/1Fnwv
Fußball Bundesliga Logo
Picha: Getty Images

Hofu hii imechochewa hasa na hatua ya klabu ya Liverpool ya Uingereza kumsajili mchezaji Robert Firmino wa Hoffenheim kwa kitita kikubwa ikilinganishwa na fedha ilizomnunua. Hoffenheim ilimsajili Firmino kwa kitita cha euro milioni 4 mwaka 2011 na kuhamia kwake Liverpool kutaipatia euro milioni 41 kwa mshambuluaji huyo kutoka Brazil na kulipiku dau la euro milioni 40, fedha ambazo Bayern Munich ililipa kumsajili mlinzi na mchezaji wa kiungo Javi Martinez.

Gazeti la Bild liliuliza katika mtandao wake Alhamisi," Je England itaifisidi Bundesliga?" na Gazeti la Suddeutsche Zeitung liliipa makala yake ya mhariri kichwa cha maneno, "Msako wa kutafuta dhahabu . "

Taarifa hiyo ikigusia kandarasi za televisheni za Ligi kuu ya England 2016-2019 itakayo gharimu euro bilioni 6.9 sawa na paundi bilioni 5.14 za Uingereza. Vilabu vya ligi kuu ya Ujerumani vitajipatia euro 835 milioni kwa msimu wa 2016-2017 wakati ambapo mkataba wa sasa wa miaka minne unaomalizika, uligharimu euro bilioni 2.51.

Englisch Premier Fussball League LOGO
Nenmbo ya Ligi kuu ya England.Picha: DW

Fedha zatawala Uingereza

Kilabu tajiri kabisa nchini Ujerumani , Bayern Munich ilichuma euro milioni 50.6 kutokana na haki miliki za televisheni za ndani nchini katika msimu uliopita. Hizo ni euro milioni 30 zaidi kuliko Paderbon ilioshuka daraja, lakini ni upungufu wa euro milioni 30 kuliko kilabu iliomaliza ligi mkiani ya Queens Park Rangers.

Haishangazi kwa hivyo kwamba Mwenyekiti wa Eintracht frankfurt Heribert Bruchhagen anaposema baada ya makubaliano na Televisheni ya England katikati ya Februari kwamba, "sijui kama Stoke City haitawasajili nusu ya wachezaji wa Borussia Dortmund au Bayer Levekusen."

Hadi sasa Stoke imetumia euro milioni 8 kumsajili mshambuliaji wa Hanover Joselu, wakati mlinzi wa FC Cologne Kevin Wimmer amejiunga na Tottenham kwa kitita cha euro milioni 7 kabla za Liverpool kutumbukiza kitita kikubwa kumpata Firmino, kutoka Hoffenheim.

Bado kuna Chelsea inayomuwania mlinzi kijana Abdul Rahman Baba ikiwa tayari kumwaga euro miloni 28. Vilabu vya England viko tayari kutumia fedha nyingi kuwasajili wachezaji kutoka ligi nyengine kwa sababu bei ya wachezaji wa ligi kuu ya Uingereza zinapanda mno, huku Rahim Sterling wa Liverpool akigharimu kiasi ya Paundi milioni 50 na Harry Kane milioni 40.

Lucas Podolski ni mmoja wa wachezaji wa Wajerumani waliohamia Ligi Kuu ya England.
Lucas Podolski ni mmoja wa wachezaji wa Wajerumani waliohamia Ligi Kuu ya England.Picha: picture-alliance/dpa/A. Di Marco

Faida itakuja kuonekana

Mchezaji wa zamani wa taifa wa England Rio Ferdinand aliandika katika mtandao wake wa Twitter," Bei kubwa za usajili wa wachezaji sasa ni kichekesho," Lakini Ferdinand mwenyewe alivunja rekodi wakati ule aliposajiliwa na Manchester united 2002 akitokea Leeds United.

Wakati timu za Uingereza zikiwania wachezaji kutoka ligi kuu ya Ujerumani, Jarida la michezo la Kickers liliandika katika uhariri wake Alhamisi, kwamba Bundesliha inaweza kufaidika kutokana na pato la fedha, na kwamba historia ya karibuni, kwa mfano pambano la kuwania taji la Ulaya Champions League 2013 kati ya Bayern Munich na Borussia Dortmund ambapo Bayern ilitawazwa mabingwa, pamoja na ubingwa wa Ujerumani wa kombe la dunia 2014, kumeonyesha kwamba Bundesliga inafanya vizuri na imegeuka kuwa kivutio.

Hilo lisiangaliwe kuwa jambo lisilo na faida , linasema jarida la michezo -Kickers, huku likiongeza kwamba, busara, elimu madhubuti, mauzo yenye faida na kiwango cha juu cha ushindani ni mambo ambayo hatimaye hulipa.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, dpae.
Mhariri: Iddi Ssessanga