Qatar iko tayari kwa mazungumzo
22 Julai 2017Katika hotuba yake ya kwanza tangu mataifa manne ya Kiarabu kuvunja uhusiano na Doha, amesema Sheikh Tamim bin Hamad al-Thani katika hali ya kukaidi kwamba maisha yanaendelea kama kawaida licha ya kile alichokieleza kuwa ni "mzingiro" usio wa haki.
Saudi Arabia , Umoja wa Falme za Kiarabu , Bahrain na Misri zilivunja uhusuiano na kuiwekea vikwazo Qatar mwezi uliopita , wakiishutumu kwa kufadhili makundi ya itikadi kali na kuunga mkono ugaidi, ambapo mfalme huyo anakana.
"Qatar inapambana na ugaidi bila kuchoka na bila kujali ni nani, na jumuiya ya kimataifa inatambua hilo,"Sheikh Tamim amesema katika hotuba yake katika televisheni.
Amezungumza masaa kadhaa baada ya waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson amesema Marekani inaridhika na juhudi za Qatar kutekeleza makubaliano yenye lengo la kupambana dhidi ya ufadhili kwa magaidi, na kuyataka mataifa hayo manne kuondoa hali ya 2kuizingira nchi hiyo".
Pia inakuja siku chache kabla ya rais wa Uturuki Recep Tayyip erdogan , ambaye anaiunga mkono Qatar katika mzozo huu, alitaajiwa kufanya ziara nchini Qatar, Saudi Arabia na Kuwait kujaribu kutatua mzozo huo.
Mapema mwezi huu wakati wa duru ya mchakato wa kufanya mazungumzo ya kidiplomasia, Tillerson alitia saini makubaliano na Qatar kupambana na dhidi ya ufadhili kwa makundi ya kigaidi, sehemu ya juhudi zinazoongozwa na Kuwait kujaribu kutatua tofauti kubwa katika mataifa washirika wakubwa wa mataifa ya magharibi katika miongo kadhaa.
Tamko rasmi kutoka kwa mataifa manne ya Kiarabu bado halijatolewa, lakini mshauri wa mfalme wa Saudi Arabia amelielezea kuwa ni tamko lililoandikwa kama na mwanafunzi. "Iwapo lingeandikwa na mwanafunzi katika shule ya msingi basi angekuwa amebahatisha tu," Saud al-Qahtani ameandika katika ukurasa wake wa Twitter.
Wachambuzi ambao wamekaribishwa na televisheni inayomilikiwa na Saudia ya al-Arabiya pia imeshutumu hotuba hiyo.
"Hii ni hotuba ya kutojihusisha ambayo inatuma ujumbe kwamba Qatar haitasitisha kuunga mkono ugaidi," amesema Ali al-naimi, mhariri wa tovuti ya habari ya mtandaoni iliyochapishwa katika Umoja wa falme za Kiarabu.
Mzozo huu unazunguka katika madai kwamba Qatar inaunga mkono makundi ya wanamgambo wa Kiislamu, ikiwa ni pamoja na Syria na Libya , na inawakumbatia wanachama wa kundi la Udugu wa Kiislamu.
Ilianzia baada ya hotuba mwishoni mwa mwezi Mei iliyotolewa na Sheikh Tamim kuonekana katika tovuti ya shirika la habari la taifa , ambalo Doha inasema hakuwahi kuitoa na kusema tovuti hiyo ilidukuliwa kutoka moja kati ya nchi jirani, ikiinyoshea kidole Umoja wa Falme za Kiarabu.
Gazeti la Washington Post, likinukuu maafisa wa ujasusi , liliripoti wiki iliyopita kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu ulipanga kudukua mitandao ya kijamii ya serikali ya Qatar na tovuti za habari ili kuweka nukuu bandia. Umoja wa Falme za Kiarabu unakana kata kata kuhusika na suala hilo.
Sheikh Tamim amevieleza vikwazo hivyo kuwa ni kampeni ambayo ilikuwa inapangwa dhidi ya Qatar , akiita hatua ya uchokozi dhidi ya sera za mambo ya kigeni za nchi hiyo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Sudi Mnette