1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Qatar yajibu masharti iliyowekewa Ghuba

3 Julai 2017

Qatar imetoa jibu lake kwa ile orodha ya masharti 13 iliyotolewa na mataifa ya Kiarabu yaliyovunja uhusiano nayo. Mataifa hayo yaliamua kuongeza muda wao wa mwisho wa kutekelezwa masharti hayo.

https://p.dw.com/p/2fqne
Katar Emir Scheich Tamim bin Hamad Al-Thani
Emir wa Qatar Tamim bin Hamad Al-ThaniPicha: picture-alliance/AP Photo/O. Faisal

Waziri wa mambo ya nje wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman al-Thani, alikutana na Emir wa Kuwait Sabah al-Ahmed, na kumuwasilishia barua iliyoandikwa na Emir wa Qatar Tamim bin Hamad, iliyokuwa na jibu la nchi yake. Haya yanajiri wakati ambapo Mfalme Salman wa Saudi Arabia ameifutilia mbali ziara yake ya kuhudhuria ule Mkutano Mkuu wa G20 wiki hii wakati ambapo nchi yake ina mzozo wa kidiplomasia na Qatar.

Yaliyokuwemo katika barua hiyo hayakujulikana mara moja, ingawa afisa mmoja wa Ghuba aliliambia shirika la habari la AFP kwamba waziri Al-Thani kweli ameiwasilisha barua hiyo katika ziara yake fupi Kuwait, ambayo imekuwa ikihudumu kama mpatanishi mkuu katika mzozo huo wa nchi hizo za Ghuba.

Mawaziri wa mambo ya nje wa Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Saudi Arabia wanatarajiwa kukutana Cairo Jumatano, kujadili hatua watakazochukua katika siku za mbeleni ili kukabiliana na Qatar.

Qatar iko tayari kujitetea

Waziri wa ulinzi wa Qatar Khalid bin Mohammed al-Attiyah, alisema nchi yake iko tayari kujitetea.

"Qatar sio nchi rahisi itakayomezwa na yeyote. Tuko tayari, tuko tayari kuitetea nchi yetu. Natumai hatutafikia hatua ambayo jeshi litahitajika kuingilia kati, lakini tuko tayari daima," alisema al-Attiyah. "Tuko hapa kuilinda nchi yetu na tutalifanya hilo. Tunafanya kazi, tunaishi kila siku kuilinda nchi yetu na tutafanya hilo."

Scheich Sabah Al-Ahmed
Emir wa Kuwait Sabah Al-AhmadPicha: Getty Images/M. Wilson

Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris Johnson kupitia taarifa aliisifu hatua ya hayo mataifa manne ya Ghuba kuongeza muda wake wa kuitaka Qatar kutimiza masharti yake na wakati huo huo, aliipongeza Qatar kwa kutoa jawabu kwa Emir wa Kuwait, akisema ni hatua muhimu ya kurejesha imani baina ya pande husika.

Huku hayo yakiarifiwa, serikali ya Ujerumani ilitangaza Jumatatu kwamba Mfalme Salman wa Saudi Arabia hatohudhuria  Mkutano Mkuu wa mataifa 20 yaliyostawi kiviwanda G20, utakaoandaliwa Hamburg wiki hii, wakati ambapo nchi yake iko katika mzozo na Qatar.

Nchi nne za Ghuba zilitangaza kusitisha uhusiano na Qatar Juni 5

Msemaji wa serikali ya Ujerumani alisema, "serikali imefahamishwa rasmi kwamba Mfalme Salman hatosafiri kuhudhuria kongamano la G20."

Kulingana na shirika la habari la DPA, Mfalme Salman mwenye umri wa miaka 81, atamtuma waziri wake wa fedha Mohammed al-Jadaan kama mwakilishi wake.

Kronprinz Mohammed bin Salman
Mfalme Salman wa Saudi Arabia hatohudhuria mkutano wa G20 HamburgPicha: picture-alliance/AP Photo/Saudi Press Agency

Saudi Arabia na nchi zengine za Ghuba zilitangaza Juni 5 zinatilia kikomo uhusiano wake na Qatar, jambo lililozua mzozo mbaya zaidi wa kidiplomasia kuwahi kulikumba eneo hilo kwa miongo kadhaa.

Nchi hizo ziliishutumu Qatar kwa kuunga mkono masuala ya itikadi kali na kuwa karibu mno na hasimu wa Saudi Arabia katika kanda hiyo, Iran, shutuma ambazo Qatar imezikataa katakata.

Nchi hizo za Ghuba tayari zimekata mawasiliano ya ndege, majini na hata ardhini na Qatar, hatua ambayo imechangia nchi hiyo kufungiwa kupata bidhaa muhimu kama chakula kutoka mataifa ya nje. Ziliwataka raia wa Qatar kuondoka katika nchi zao na zikachukua hatua kadhaa dhidi ya kampuni za Qatar na taasisi zake za kifedha.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/DPAE/APE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman