RABAT: Wahamiaji wavuka mpaka kinyume na sheria
5 Oktoba 2005
Kwa mara ya tano katika kipindi cha wiki moja,wahamiaji wa Kiafrika nchini Morocco wameweza kuvuka nyuzio zenye ncha kali na kukimbilia eneo la Hispania Melilla kaskazini mwa Afrika.Hadi wahamiaji 30 walivuka mpaka usiku wa kuamkia leo.Siku ya jumatatu Waafrika 350 walijipenyeza Melilla katika jeribio la kutaka kukimbilia Ulaya.Umoja wa Ulaya ukijibu tukio hilo,umeamua kutuma wataalamu kuchunguza hatua za ukaguzi kwenye mpaka wa Morocco.Waziri wa sheria na usalama wa Umoja wa Ulaya,Franco Frattini amesema gharama zitasismamiwa pia na Umoja wa Ulaya.Morocco kwa upande wake iwachukuwe hao watu waliojaribu kuhamia Ulaya kinyume na sheria.Wiki iliyopita Waafrika 5 walipoteza maisha yao walipojaribu kukimbilia eneo jingine la Hispania Ceuta.Hispania imechapuza kazi za kuimarisha nyuzio kwenye mipaka yake.Kwa Morocco na nchi zingine za Afrika Kaskazini zinasema nchi za Kiafrika,kusini mwa jangwa la Sahara zinahitaji misaada zaidi kutoa nafasi za ajira ili watu wanaofikiria kuhamia kwengine,watabakia makwao badala ya kujaribu kwenda Ulaya.