Raia Uganda wahofia uchaguzi mkuu ujao utakumbwa na ghasia
7 Septemba 2020Katika zoezi lililofanyika kote nchini mwishoni mwa wiki, wagombea kadhaa walishuhudiwa wakishiriki katika kuwashambulia wapinzani na wafuasi wao ikiwemo waziri mmoja kusababisha kifo cha mtu baada ya kumpiga risasi.
Kwa kuwa chama tawala cha NRM kina ufuasi mkubwa sehemu mbalimbali za nchi, zoezi la uchaguzi wa washika bendera liliwahusisha angalau theluthi tatu ya wapiga kura waliopanga milolongo nyuma na wagombea au picha zao katika vituo mbalimbali vya kupigia kura. Hali hii ilichangia pakubwa kuondosha udanganyifu kwani ilikuwa dhahiri nani alikuwa ameshinda.
Lakini hali baadaye iliishia katika ghasia sehemu mbalimbali za nchi wakati wa kutangazwa kwa matokeo. Hii ilitokana na wasimamizi fulani kubadili matokeo kinyume na ilivyokuwa kwenye zoezi lenyewe.
Aidha visa vya vitisho vilivyowahusisha hata wanajeshi, kuwahonga wapigaji kura kwa pesa na kubadilishwa kila mara kwa madaftari ya wapigakura ni miongoni mwa yale yanayodaiwa kusababisha vurugu katika zoezi hilo.
Sikiliza pia: MAONI-Hali nchini Uganda, kuelekea uchaguzi wa 2021.
Licha ya makundi ya wafuasi kupinga utaratibu uliofuatwa katika kila hatua, wagombea wengi waliokuwa wakitetea kuhifadhi nafasi zao walishindwa katika uchaguzi huo.
Miongoni mwa walioshindwa ni mawaziri na wanasiasa mashuhuri wa muda mrefu. Katika mojawapo ya visa waziri wa masuala ya wafanyakazi alinaswa video kwenye simu akiwashambulia wafuasi wa mpizani wake.
Mmoja kati ya wafuasi hao alifariki baadaye akipata matibabu na waziri huyo aliwahi kushikilia wadhifa wa naibu mkuu wa sheria amekamatwa pamoja na walinzi wake. Vifo vingine vinne vinavyodaiwa kutokana na uchaguzi huo viliripotiwa kutoka sehemu zingine za nchi. Mazingira haya ndiyo yamepelekea wananchi mbalimbali kuhofia hali itakavyokuwa katika uchaguzi mkuu ujao.
Soma pia: Bobi Wine azindua chama kipya cha siasa kabla ya uchaguzi
Ikumbukwe kuwa safari hii waangalizi wa kimataifa hawatarajiwi kuja kufuatilia mchakato wa uchaguzi. Wakati wa kuendesha zoezi hilo, kanuni za kuepusha kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19 zilikiukwa pakubwa pale makundi ya wafuasi yaliposhuhudiwa yakisherehekea ushindi wa wagombea wao huku wengi wakiwa hawajavalia barakoa.
Hili limesababisha wafuasi wa upinzani kuhoji kwa nini wao husambaratishwa na polisi wakitumia nguvu za kupindukia lakini haikuwa hivyo kwa wafuasi wa chama tawala.
Kingine kilichoshuhudiwa katika uchaguzi huo ni kujitokeza kwa ndugu, wana na jamaa za wanasiasa mashuhuri kugombea tiketi za chama cha NRM. Kwa mfano ndugu mdogo wa rais Museveni anachuana na binti wa waziri wa masuala ya kigeni Sam Kutesa katika zoezi lililoahirishwa kwa kuhofia kutokea kwa vurugu nyingi.