1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Haiti akamatwa akihusishwa na mauaji ya Rais Moise

12 Julai 2021

Polisi nchini Haiti imesema imemkamata raia wa nchi hiyo aliyetumia ndege binafsi kushirikiana na watu wanaotuhumiwa kupanga na kutekeleza mauaji ya Rais wa Haiti, Jovenel Moise.

https://p.dw.com/p/3wLcx
Haiti | PK Polizeichef Léon Charles
Picha: AFP via Getty Images

Mkuu wa Polisi wa Haiti, Leon Charles amemtambulisha mtuhumiwa huyo kama Christian Emmanuel Sanon, mwenye umri wa miaka 63 anayeishi Florida, Marekani. Amesema alikwenda Haiti kwa kutumia ndege binafsi mwanzoni mwa mwezi Juni akiwa na walinzi binafsi na alitaka kuchukua nafasi ya urais.

Mkuu huyo wa polisi hakueleza nia ya Sanon, zaidi ya kusema zilikuwa kisiasa na kwamba aliwasiliana na mtuhumiwa mmoja baada ya kukamatwa. Charles amewaambia waandishi habari kwamba nia ya washambuliaji hao awali ilikuwa kuhakikisha usalama wa Sanon, lakini baadae lengo lilibadilishwa na walimpa mmoja wa wauaji hati ya kumkamata rais na kwamba maafisa wa polisi walipata vitu kadhaa kwenye nyumba ya Sanon.

Vitu vilivyokutwa ndani ya nyumba

''Ndani ya nyumba ya Christian Emmanuel Sanon, tumepata kofia yenye nembo ya Mamlaka ya Kupambana na Biashara Haramu ya Madawa nchini Marekani, DEA, masanduku sita ya kuwekea bunduki, maboksi 20 yenye risasi, vibao vinne vyenye namba za magari zilizosajiliwa kwa namba za Jamhuri ya Dominika, magari mawili na mawasiliano aliyofanya na watu wasiojulikana," alifafanua Charles.

Charles amesema jumla ya raia 26 wa Colombia wanatuhumiwa kumuua Rais Moise Jumatano iliyopita. 18 kati yao wamekamatwa pamoja na raia wawili wenye uraia wa Haiti na Marekani. Amesema bado wanaendelea kuwasaka watuhumiwa watano na kwamba watuhumiwa watatu wameuawa.

Haiti - Ermordung des Präsidenten Jovenel Moise
Baadhi ya wananchi wakiandamana nje ya kituo cha polisi Port-Au-Prince kupinga mauaji ya MoisePicha: Richard Pierrin/Getty Images

Mkuu huyo wa polisi wa Haiti amesema wanashirikiana na maafisa wa ngazi ya juu wa Colombia kubaini taarifa zaidi za wanaotuhumiwa kupanga mauaji hayo, na kuangalia lini waliondoka Colombia na nani alilipia tiketi zao.

Wakati huo huo, kundi la watu wanaotuhumiwa kwa mauaji ya Rais Moise limewaambia wapelelezi kwamba walitaka kumkamata kiongozi huyo na sio kumuua. Hayo yamebainika katika ripoti iliyotolewa siku ya Jumapili na gazeti la Marekani la Miami Herald. Likiwanukuu watu waliozungumza na watuhumiwa 19 wanaoshikiliwa hadi sasa, gazeti hilo limeeleza kuwa lengo lao lilikuwa kumkamata Moise na kumpeleka kwenye Ikulu ya rais.

Baadhi ya watuhumiwa walikuwa wakalimani

Duru za karibu na intelijensia zimesema watuhumiwa wawili wenye uraia wa Haiti na Marekani, James Solages na Joseph Vincent wamewaambia wapelelezi kwamba walikuwa wakalimani wa kitengo cha makamandoo wa Colombia ambacho kilikuwa na hati ya kumkamata Moise. Lakini walipofika walimkuta keshakufa.

Miami Herald, limesema raia wa Colombia wanaoshikiliwa wamesema walitumwa kufanya kazi Haiti na kampuni ya ulinzi ya CTU yenye makao yake Miami, inayoendeshwa na muhamiaji wa Venezuela, Antonio Emmanuel Intriago Valera. CTU wala Intriago hawakuweza kupatikana mara moja kujibu madai hayo.

Wananchi wa Haiti katika maeneo ya mji mkuu Porto-Au-Prince wamepanga kuandamana wiki hii kupinga mauaji ya Moise na kumpinga waziri mkuu wa mpito na anayeiongoza nchi kwa sasa, Claude Joseph.

(AP, AFP, DPA, Reuters)