Raia wa kigeni waikimbia Libya
24 Februari 2011Hali nchini Libya imeendelea kuwa ya wasi wasi wakati kiongozi wa nchi hiyo kanali Muammar Gaddafi akijaribu kurejesha udhibiti wa mji mkuu Tripoli pamoja na maeneo ya magharibi. Mashariki mwa nchi hiyo, wanajeshi wa serikali wameamua kuunga mkono upande wa upinzani na wamejiunga na waandamanaji ambao wamechukua udhibiti wa eneo hilo.
Katibu mkuu wa umoja wa mataifa , Ban Ki-moon , amesema kuwa anaangalia matukio katika nchi hiyo kwa wasi wasi mkubwa. Wakati huo huo, umoja wa Ulaya na Marekani zimeshutumu ghasia hizo zinazoendelea ambazo zimesababisha watu karibu 300 kuuwawa. maelfu ya raia wa kigeni wanajaribu kuikimbia nchi hiyo kwa njia zozote zinazopatikana. Jana Jumatano jioni , ndege mbili za Ujerumani ziliwasili katika viwanja vya ndege vya Frankfurt na Kolon kutoka Tripoli zikiwa na idadi kadha ya Wajerumani ambayo haikutajwa, pamoja na raia wengine wa mataifa ya Ulaya.