1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Mali wapiga kura katika uchaguzi wa bunge

24 Novemba 2013

Raia wa Mali wanapiga kura leo Jumapili (24.11.2014) katika uchaguzi wa bunge unaolenga kuisaidia nchi hiyo inayokabiliwa na msukosuko kurejea katika mkondo wa demokrasia.

https://p.dw.com/p/1AN6y
Karatasi ya kura na picha ya mmoja wa wagombea wa ubunge Mali Yu Hong Wei maarufu kama Astan Coulibaly
Karatasi ya kura na picha ya mmoja wa wagombea wa ubunge Mali Yu Hong Wei maarufu kama Astan CoulibalyPicha: abamako.com

Uchaguzi huo hata hivyo umegubikwa na kitisho cha mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka kwa wanamgambo wenye itikadi kali za kiislamu. Aidha unaashiria hatua za kwanza za kufufuka taifa hilo la Afrika Magharibi baada ya kutumbukia katika msukosuko kutokana na mapinduzi ya jeshi mwezi Machi mwaka jana, na kumalizia mchakato ulioanza kwa kuchaguliwa rais wa kwanza baada ya mzozo huo mnamo mwezi Agosti.

Takribani raia milioni 6.5 wana kibali cha kupiga kura kulichagua bunge jipya, huku kukiwa na wagombea 1,000 wanaowania viti 147. lakini shughuli ya upigaji kura inafanyika wakati kuwa na ongezeko la machafuko kutoka kwa waasi walio na mafungamano na al-Qaeda ambao wanaendesha harakati zao kaskazani mwa nchi hiyo, na kusababisha kitisho kwa wanajeshi wa Ufaransa na Afrika waliopewa jukumu la kuweka ulinzi katika uchaguzi huo pamoja na jeshi la Mali.

Majeshi ya Ufaransa yalishuhudia shambulizi lao la kwanza katika mji mkuu Bamako Ijumaa iliyopita, wakati ofisa wa polisi anayefanya kazi na jeshi alipobahatika kunusurika majeraha mabaya baada ya mtu aliyekuwa na bunduki na kumfyatulia risasi. Siku moja kabla, wanamgambo waliushambulia mji wa kaskazini wa Gao, ijapokuwa makombora yao hayakuweza kufika katika maeneo ya mijini.

Rais wa Mali Ibrahim Boubacar Keita
Rais wa Mali Ibrahim Boubacar KeitaPicha: Reuters

Wiki tatu za kampeni za uchaguzi hazikushika moto nchini Mali, na wachambuzi wanatabiri idadi ndogo ya wapiga kura isiyofikia asilimia 50 iliyojitokeza katika uchaguzi wa rais ambao waziri mkuu wa zamani Ibrahim Boubacar Keita aliibuka mshindi.

Chama tawala cha Rally for Mali – RPM kimeahidi kupata “wingi wa kutosha wa viti” ili kuitengeneza barabara ya mageuzi ambayo Keita anapanga kuweka ili kuujenga upya uchumi wa Mali uliokwama na kupunguza mivutano ya kikabila kaskazini mwa nchi hiyo.

Lakini mtalaamu wa sayansi ya kijamii mjini Bamako Mamadou Samake ameliambia shirika la habari la AFP kuwa itakuwa “vigumu au lisilowezekana” kwa chama chochote kimoja cha kisiasa kupata moja kwa moja wingi wa kutosha wa viti bungeni, akibashiri kuwa chama cha RPM kitahitaji kuingia katika muungano ili kuunda serikali.

Uchaguzi huo utasimamiwa na mamia ya waangalizi wa Mali na Kimataifa ikiwa ni pamoja na ujumbe wa Umoja wa Ulaya na timu ya maafisa 100 kutoka Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi - ECOWAS.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Sekione Kitojo