Raia wakimbia kutoka Ghouta mashariki
17 Machi 2018Vifo hivyo vya hivi karibuni kabisa vimefikisha idadi jumla ya mashambulizi yaliyodumu karibu mwezi mmoja kufikia watu 1,350, huku mataifa makubwa duniani bado yakishindwa kuzuwia moja kati ya mizozo mibaya kabisa iliyosababisha uharibifu.
Vita nchini Syria vinaingia mwaka wa nane kwa mashambulizi mengine yanayosababisha mauaji yakijitokeza pia upande wa kaskazini, ambako majeshi yanayoongozwa na Uturuki yameendelea na mashambulizi kulikamata jimbo linaloishi Wakurdi wengi la Afrin.
Operesheni hiyo imesababisha maelfu ya watu kukimbia, huku mashambulizi ya mabomu dhidi ya mji wa Afrin jana Ijumaa yakiuwa watu 43, theluthi yao wakiuwawa katika mashambulizi ya anga katika hospitali.
Ukingoni mwa mji wa Ghouta, eneo kubwa linaloishi watu wa vijijini likiwa umbali mfupi kutoka Damascus na rahisi kufika makombora, zaidi ya raia 2,400 walikimbia kutoka katika miji iliyoharibiwa, wakibeba vitu vichache katika mifuko na vilivyofungwa katika nguo.
Makundi ya watu yalijikusanya katika vituo vya serikali nje kidogo ya Ghouta mashariki jana Ijumaa, wakiwa hawana uhakika watafanya nini baada ya hapo baada ya kuingia moja kwa moja katika udhibiti wa majeshi ya serikali ambayo yamekuwa yakishambulia bila kukoma nyumba zao kwa wiki kadhaa.
"Tulikuwa tuna hofu ya kuondoka, walituambia jeshi litatukamata," alisema Abu Khaled mwenye umri wa miaka 35, ambaye alikuwa akifanya biashara ya kuuza nguo mjini Ghouta.
"Tulikutana na jeshi na hatukuona hivyo, lakini sasa kimsingi tunaishi kambini," aliliambia shirika la habari la Ufaransa AFP.
Watu wengi zaidi wamekimbia
Balozi wa Syria katika Umoja wa Mataifa Bashar al-Jaafari amesema watu 40,000 wamekimbia kutoka Ghouta siku ya Alhamis, na hatua hiyo ya kukimbia watu kwa wingi inaonekana kutokea bila ya serikali kujitayarisha.
Misururu mirefu ya watu ilionekana nje ya vyoo vya umma, na familia zilizokimbia makaazi yao zililalamikia kukosekana kwa maji ama magodoro.
Katika ujumbe uliotangazwa kupitia televisheni ya taifa jeshi la Syria liliwataka raia wote kutumia eneo maalum lililotengwa na jeshi hilo kuondoka kutoka katika eneo hilo, likisema limekamata asilimia 70 ya ardhi iliyokuwa ikidhibitiwa na waasi.
Mashambulizi ya ardhini yaliyokuwa yakifanywa na jeshi la Syria pamoja na wanamgambo washirika wao yameligawa eneo la Ghouta mashariki katika sehemu mbali mbali, kila moja likiwa linashikiliwa na kundi tofauti.
Yale makundi matatu ya wapiganaji wa Kiislamu yamesema jana Ijumaa yatakuwa tayari kufanya majadiliano ya moja kwa moja na Urusi kuhusiana na usitishaji mapigano katika Ghouta, lakini hayakutaja mazungumzo na serikali ya Syria.
Taarifa yao imekuja masaa machache baada ya mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria Staffan de Mistura kusema mazungumzo yanaendelea kati ya Urusi na moja kati ya makundi, Jaish al-Islam.
Mazungumzo hayo tayari yamesababisha kuwapo na siku sita za utulivu katika mji mkubwa wa eneo la Ghouta wa Douma. Mji wa Douma pia ulishuhudia upelekaji wa chakula, na mamia ya raia walipata usafiri wa mabasi kuondoka kutoka katika mji huo kama sehemu ya kuwaondoa watu kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Yursa Buwayhid