Raia waondolewa kisiwani Tenerife kufuatia moto wa nyika
19 Agosti 2023Mamlaka katika kisiwa cha Tenerife nchini Uhispania, zimelazimika kuwahamisha wananchi zaidi kutoka kwenye makaazi yao, wakati moto wa nyika ukizidi kusambaa kaskazini mwa kisiwa hicho.
Maafisa wanasema hali ya joto kali, ukame na upepo vimechangia moto huo kushindwa kudhibitiwa katika Visiwa vya Canary. Afisa mmoja wa eneo hilo Manuel Miranda amesema wamelazimika kuwahamisha wananchi kutokana na kitisho na hatari ya moto huo kuwa karibu.
Moto wa msituni wazusha sokomoko kusini mwa Ulaya
Moto huo ulizuka siku ya Jumatano katika hifadhi ya taifa karibu na kilele cha Mlima wa Volkanao wa Teide. Akizungumza Ijumaa jioni, kiongozi wa mkoa Fernando Clavijo alisema hekta zipatazo 5,000 zimeteketea kwa moto na watu wapatao 4,000 wamehamishwa.
Hadi sasa, maeneo maarufu ya watalii kisiwani humo hayajaathiriwa na viwanja vya ndege vyote vya Tenerife vilikuwa vikifanya kazi kama kawaida.