Rais Adama Barrow atangazwa mshindi wa urais Gambia
6 Desemba 2021Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Alieu Momarr Njai jana alimtangaza Barrow kuwa mshindi, katika matokeo ya mwisho saa chache baada ya wagombeaji wa upinzani kupinga matokeo ya awali yaliyompa Barrow nafasi ya kuongoza.
Uchaguzi wa Gambia uliofanyika Jumamosi ni wa kwanza tangu kiongozi wa kimabavu na wa zamani Yahya Jammeh alipokimbia nchi. Uchaguzi huo unachukuliwa kama kipimo cha demokrasia changa ya taifa hilo.
Mkuu wa ujumbe wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), Ernest Bai Koroma ametoa wito kwa wagombea wote kukubali matokeo ya uchaguzi kwa nia njema.
Kwenye taarifa ya pamoja mpinzani mkuu Darboe na wagombea wengine wawili walisema wamekataa matokeo yaliyotangazwa na hatua yoyote iko mezani kuchukuliwa.
Uchaguzi huo unatazamwa kwa karibu kama mtihani wa mabadiliko ya kidemokrasia nchini Gambia, ambapo Jammeh alitawala kwa miaka 22 baada ya kutwaa madaraka katika mapinduzi yasiyo ya umwagaji damu mwaka 1994.