1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Adama Barrow kurejea nchini Gambia

23 Januari 2017

Barrow atarejea kutoka Senegal kuchukua hatamu za uongozi nchini Gambia. Wakati huo huo, Yahya Jammeh alaumiwa kwa kuiba mamilioni ya dola kutoka kwenye hazina kuu kabla ya kuondoka

https://p.dw.com/p/2WF4F
Gambia Machtwechsel - Präsident Adama Barrow in Dakar, Senegal
Picha: Reuters/S. Shadid

Rais huyo wa zamani wa Gambia Yahya Jammeh hatimae aliondoka nchini humo na kufikisha mwisho wa utawala wake wa miaka 22. Amekwenda Guinea ya Ikweta pamoja na familia yake. Vikosi vya majeshi ya Afrika Magharibi viliingia nchini Gambia hapo jana na kupokelewa kwa shangwe na nderemo kutoka kwa raia wa Gambia.

Afisa mmoja wa jeshi la Senegal amesema kuwa hawakupata upinzani wowote kutokana na kauli ya mkuu wa Jeshi la Gambia Ousman Badije kutangaza kuwa anamuunga mkono rais mpya Adama Barrow. Vikosi hivyo vitakuwa na jukumu la kulinda usalama wa rais mpya ambaye bado yuko nchini Senegal kwa zaidi ya wiki sasa.  

Ex-Präsident Jammeh verlässt Gambia
Aliyekuwa Rais wa Gambia Yahya Jammeh akiondoka GambiaPicha: Picture-Alliance/dpa/J. Delay

Wakati huo huo, msaidizi wa rais mpya wa Gambia Mai Ahmed Fatty amesema hazina ya Gambia imebaki tupu kutokana na hivi karibuni kuibiwa kwa takriban dola milioni 11. Amefahamisha kuwa Jammeh alitoa kiasi hicho cha fedha wiki mbili zilizopita.
 
Fatty amesema kuwa wakati ambapo Barrow anatarajiwa kuchukua hatamu za uongozi, nchi ya Gambia inakabiliwa na hali mbaya kifedha. Wakosoaji wameeleza wasiwasi wao kutokana na tamko la Umoja wa mataifa, Jumuiya ya ushirikiano wa kiuchumi ya Afrika Magharibi ECOWAS pamoja na Umoja wa Afrika ambapo wanasema tamko hilo linamuhakikishia Jammeh kuwa maslahi yake pamoja na yale ya familia yake yatalindwa.

Tamko hilo linamlinda Yahya Jammeh kwa kila hali kuanzia mali zake hadi utu wake, ijapokuwa wataalamu wanasema kuwa agizo hilo halikuambatanishwa kisheria. Guinea ya Ikweta  haikutia saini mkataba wa Roma hivyo basi haitawajibika kumpeleka Jammeh iwapo atafunguliwa mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita na maovu dhidi ya binadamu ya ICC huko mjini The Hague.  

Wanajeshi wa ECOWAS watashirikiana na vikosi vya usalama vya Gambia kuhakikisha kuwa ikulu ya Banjul iko salama kwa ajili ya Rais mpya Adama Barrow. Vile vile, makaazi ya Jammeh yaliyopo katika mji wa Kanilai yatachunguzwa kwani inaaminiwa kuwa rais huyo wa zamani ameficha silaha na pengine makundi ya wafuasi wake huenda yakawa yamejificha katika eneo hilo.  

Mwandishi: Zainab Aziz/AFPE/DPAE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman