1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ousmane Sonko ateuliwa kuwa Waziri Mkuu Senegal

Angela Mdungu
3 Aprili 2024

Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye, amemteua mwanasiasa maarufu wa upinzani Ousmane Sonko kuwa Waziri Mkuu wa taifa hilo. Ametangazwa kushika wadhifa huo baada ya Dioumaye Faye kuapishwa kuwa Rais wa Senegal Jumanne.

https://p.dw.com/p/4eNdR
Ousmane Sonko, alikuwa mpinzani mkubwa wa Macky Sall
Waziri Mkuu wa Senegal Ousmane SonkoPicha: Sylvain Cherkaoui/AP/dpa

Ousmane Sonko, aliyekuwa mpinzani mkuu wa rais aliyemaliza muda wake Macky Sall ni maarufu miongoni mwa vijana wengi wa mataifa ya Afrika ya Magharibi. Taarifa ya kutangazwa kwake kuwa Waziri Mkuu imetolewa na katibu mkuu wa rais Oumar Samba Ba kupitia televisheni ya taifa. Akizungumza baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo Sonko amesema hawezi kumuacha Rais Faye abebe mwenyewe jukumu kubwa alilonalo la kuiongoza nchi.

Soma zaidi: Rais mteule wa Senegal aapishwa, aahidi mabadiliko

Akizungumza baada ya kuteuliwa kwake, Sonko mwenye miaka 49 ameongeza kuwa jukumu hilo la uwaziri Mkuu ni zito kwani llinahusisha kuongoza timu itakayokuwa na kibarua cha kufanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo kama sehemu ya sera ya taifa.

Zaidi ameongeza kuwa katika saa chache zijazo atapeleka kwa Rais Bassirou Faye mapendekezo ya majina ya wanawake na wanaume watakaokuwa mawaziri, manaibu wa mawaziri au makatibu wa kuu wa serikali watakaofanya kazi kwa ajili ya umma na si kujinufaisha kutokana na madaraka yao, kama ilivyoainishwa katika katiba.

Aahidi kufanya kazi kwa uwazi

Kiongozi huyo aliyewahi kuwa afisa wa zamani wa masuala ya kodi kama ilivyo kwa Rais Faye, ameahidi kufanya kazi kwa uwazi mkubwa. Awali, Waziri Mkuu huyo mpya wa Senegal  alizuiwa kushiriki katika uchaguzi wa Machi 24 kutokana na kuhukumiwa kifungo jela kutokana na tuhuma kadhaa zilizokuwa zikimkabili.

Senegal Dakar | Ousmane Sonko ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Senegal
Ousmane Sonko baada ya kuachiliwa kutoka jela hivi karibuniPicha: Abdou Karim Ndoye/REUTERS

Sambamba na Faye, Sonko ni miongoni mwa kundi la wanasiasa wa upinzani walioachiliwa huru kutoka jela, siku 10 kabla ya uchaguzi. Itakumbukwa kuwa Sonko Alimchagua Faye kuwa mbadala wake katika kinyang'anyiro hicho cha uraisi.

Wafuasi Sonko wameendelea kushikilia msimamo kuwa, matatizo ya kisheria yaliyokuwa yakimuandama yalilenga kumuondoa katika kinyang'anyiro hicho cha Urais. Hata hivyo Sonko na Rais wa sasa Bassirou Diomaye, Faye walifanya kampeni ya pamoja iliyokuwa imebeba kaulimbiu iitwayo "Diomaye ni Sonko" ambapo Sonko aliwaomba wafuasi wake wamuunge mkono Faye.