Wajadili uhasama miongoni mwao
14 Aprili 2016Wakuu wa serikali na viongozi wa nchi zaidi ya 30 kutoka shirika la ushirikiano la nchi za kiislamu, OIC , wanaanza mkutano wa kilele wenye lengo la kuziondoa tofauti baina ya nchi za kiislamu.
Mazungumzo ya viongozi hao pia watajadili masuala ya Palestina,Libya na Nargono Karabakh.
Mwenyeji wa mkutano huo, Uturuki imesema inakusudia kuitumia fursa ya mkutano huo ili kujaribu kupunguza tofauti zilizopo miongoni mwa Waislamu wanaokadiriwa kufikia Bilioni 1.7 duniani.
Yemen na Syria kugubika mazungumzo
Hata hivyo wachunguzi wanaamini migogoro ya Syria na Yemen inaweza kuyagubika mazungumzo yanayofanyika chini ya uenyekiti wa Rais Tayyip Erdogan. Miongoni mwa viongozi muhimu wanaohudhuria mkutano huo wa kilele mjini Istanbul ni Mfalme wa Saudi Arabia, Salman na Rais wa Iran Hassan Rouhani.
Saudi Arabia na Iran zinatafautiana juu ya migogoro ya Syria na Yemen. Rais wa Iran Rouhani aliewasili jana mjini Istanbul pia anatarajiwa kufanya mazungumzo na wenyeji wake wa Uturuki.
Hata hivyo wakati mkutano huo ni muhimu viongozi wenye uzito wa juu kama Mfalme wa Jordan Abdullah na Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi hawatakuwapo. Uhusiano baina ya Uturuki na Misri bado haujarejea katika hali nzuri tangu kuondolewa madarakani kwa aliekuwa Rais wa Misri Mohammed Mursi mnamo mwaka 2013. Mursi alikuwa mshirika mkubwa wa Uturuki.
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu amesema mkutano wa mjini Istanbul unafanyika wakati ambapo jumuiya ya nchi za kiislamu inakabiliwa na migogoro mingi.
Waziri Cavusoglu amesema umwagikaji damu miongoni mwa ndugu katika nchi za kiislamu ni jambo linalosababisha machungu.Hata hivyo Waziri huyo ameelezea matumaini kwamba mkutano wa viongozi wa nchi 57 za kiislamu-OIC, unaoendelea mjini Istanbul utatoa mchango katika juhudi za kuondosha uhasama.
Kabla ya mkutano kuanza, Mfalme wa Saudi Arabia Salman alifanya ziara iliofungua ukurasa mpya katika uhusiano baina ya Saudi Arabia na Uturuki.Rais Erdogan alimlaki Mfalme huyo kwenye uwanja wa ndege wa Esenboga.
Katika ishara ya kuimarika kwa uhusiano baina ya nchi hizo mbili, Rais Erdogan alimtunukia Mfalme Salman medali ya heshima ya juu ya nchini Uturuki. Uturuki na Saudi Arabia zinakubaliana kwamba mgogoro wa Syria utaweza kutatuliwa ikiwa Rais Bashar al-Assad ataondoka madarakani. Uturuki na Saudi Arabia pia zinawaunga mkono waasi wanaopambana na utawala wa Assad.
Mwandishi: Mtullya Abdu./afp,rtre/
Mhariri: Grace Patricia Kabogo