Rais Erdogan asema shambulizi ni mbinu ya kuigawanya Uturuki
4 Januari 2017Katika matamshi yake ya kwanza hadharani kuhusiana na shambulizi la mkesha wa mwaka mpya katika kilabu cha Reina mjini Istanbul, aliyoyatoa katika ikulu ya rais hii, Rais Erdogan alisema kuwa lengo la shambulizi hilo liko wazi la kutaka kuleta mgawanyiko katika nchi hiyo. Rais huyo aliongeza kuwa, ''hakuna mfumo wa mtu yeyote unaokumbwa na hatari. Hatuwezi kuruhusu jambo hilo kutokea. Katika miaka 14 madarakani, hatujawahi kutoa fursa ya suala kama hilo.''
Aliendelea kusema kuwa, ''mashambulizi haya yananuwia kutufanya kuweka hisia zetu mbele ya fikra,'' na kuongeza kuwa hata hali hii itakaposababisha mateso, haiwezi kuwa sababu ya kubadilisha mawazo.
Serikali yasema imemtambua mshambuliaji
Huko hayo yakijiri, serikali ya Uturuki imesema kuwa imemtambua mshambuliaji wa shambulizi hilo la Istanbul lililosababisha mauaji ya watu 39. Haya yalisemwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu wakati wa mahojiano na shirika la habari la Anadolu linalomilikiwa na serikali bila kutoa jina la mshambuliaji huyo. Cavusoglu aliendelea kusema kuwa juhudi za kumkamata zinaendelezwa na kwamba nyumba alimoishi mshukiwa huyo imefanyiwa uchunguzi na kwamba shambulizi hilo lilipangwa kwa njia ya kitaalamu.
Kwa mara ya kwanza, kundi la wanamgambo la dola la kiislamu lilidai kutekeleza shambulizi kubwa kama hilo nchini Uturuki.
Kulingana na shirika la habari la Anadolu, katika mji wa Magharibi wa Izmir, takriban watu 20 ikiwa ni pamoja na wanawake 11 wamezuiliwa kama sehemu ya uchunguzi kuhusiana na shambulizi hilo.
Shirika hilo lilisema kuwa watu hao ni wa asili ya Arabuni ya Kati na Syria huku shirika la habari la Dogan likisema kuwa ni watu kutoka familia tatu.
Inadaiwa kuwa baadhi ya wale wanaozuiliwa waliishi na mshukiwa wa shambulizi hilo katika nyumba moja huko Konya.
Kukamatwa kwa watu hao kunapelekea idadi ya wale wanaozuiliwa na polisi kuwa 36 kufikia sasa ikiwa ni pamoja na raia wawili wa kigeni.
Mwandishi: Tatu Karema/ AFPE/ RTRE
Mhariri: Grace Patricia Kabogo