1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Jacob Zuma asubiriwa atangaze kujiuzulu

Isaac Gamba
14 Februari 2018

Ofisi ya rais nchini Afrika Kusini imevieleza vyombo vya habari leo Jumatano kusubiri taarifa kuwa huenda rais Jacob Zuma akaongea na vyombo vya habari kuhusianan na hatua ya kujiuzulu.

https://p.dw.com/p/2sexf
Südafrika Präsdient  Jacob Zuma
Picha: Reuters/S. Sibeko

Taarifa ya ofisi ya rais imekuja huku vyombo vya habari vikiripoti kuwa rais Jacob Zuma atalihutubia taifa baadaye hii leo ili kujibu wito wa chama tawala cha ANC kuwa analazimika kujiuzulu kama rais wa nchi hiyo.

Chama cha African National Congress ( ANC ) kimesema hapo jana kuwa kimeamua kumtaka rais Zuma aachie madaraka  lakini hakikumpa muda maalumu wa kufanya hivyo huku katibu mkuu wa chama hicho Ace Magashule akisema halmashauri kuu ya taifa ya chama cha ANC imegawanyika  kuhusiana na lini hasa Zuma atapaswa kujiuzulu ingawa chama hicho kilitarajia aitikie mwito huo wa kujiuzulu leo Jumatano.

Waziri wa fedha Malusi Gigaba amelieleza shirika la habari la CNN kuwa rais Jacob Zuma alikuwa anatarajiwa kulihutubia taifa baadaye hii leo na kuwa wanatarajia ataamua kilicho sahihi.

Hata hivyo msemaji wa rais Jacob Zuma hakupatikana kutoa ufafanuzi na pia hakukuwa na uthibitisho rasmi kutoka kwa rais iwapo hotuba ya kiongozi huyo itatolewa hii leo.

Ndugu wa mfanyabiashara Gupta watiwa mbaroni

Südafrika Polizei durchsucht Anwesen von Präsident Zumas Günstlingen
Picha: Reuters/J. Oatway

Hayo yanajiri huku polisi nchini Afrika Kusini hii leo wakiwatia mbaroni watu watatu wa familia ya mfanyabiashara maarufu nchini humo Gupta anayehusishwa na kashifa za kifisadi ambazo pia zinadaiwa kumuhusisha rais Jacob Zuma.

Maafisa wa polisi waliokuwa na sialaha nzinto leo Jumatano wamevamia makazi ya kifahari ya familia ya Gupta kufuatia madai kuwa ndugu hao wa tatu wanahusishwa na kashifa za kifisadi ambazo pia zinamkabili Zuma ambaye amemualiwa na chama chake ajiuzulu.

uma tayari anakabiliwa na hoja bungeni ya kupigiwa kura ya kutokuwa na imani naye ambayo iliwasilishwa na upinzani  na kura hiyo  imepangwa kufanyika Februari 22.

Chama cha ANC kinaweza kutumia nguvu yake kuunga mkono hoja hiyo iwapo Zuma ambaye amenusurika mara kadhaa kuondolewa madarakani kupitia kura hiyo atakataa kujiuzulu na baraza lake la mawaziri nalo pia litalazimika kujiuzulu iwapo kura hiyo itaitishwa.

Rais Jacob Zuma amekuwa akikabiliwa na kashifa kadhaa tangu alipoingia madarakani mwaka 2009 huku uchumi wa Afrika Kusini ukidorora katika kipindi cha utawala wake na mabenki pamoja na makampuni ya madini yakisita kuwekeza kutokana na mashaka kuhusiana na sera za nchi hiyo  ikiwa ni pamoja na kukithiri kwa rushwa.

Shinikilizo la kisiasa limeongezeka dhidi yake tangu makamu wake Cyril Ramaphosa alipochaguliwa  Disemba mwaka jana kuwa kiongozi wa chama  ANC kilichoasisiwa miaka 106  iliyopita.

Ramaphosa alimshinda Nkosazana Dlamini-Zuma , mke wazamani wa rais Zuma  kwa asilimia chache ya kura katika uchaguzi ndani ya chama hicho wa mwaka jana.

Mwandishi: Isaac Gamba/rtre/dpae

Mhariri: Iddi Ssessanga