Rais Karzai wa Afghanistan ziarani Marekani
7 Januari 2013Rais Hamid Karzai wa Afghanistan ameondoka Kabul kuelekea Marekani ambako anatazamiwa kusalia kwa siku kadhaa.Amepangiwa kuzungumza na kiongozi mwenzake wa Marekani,Barack Obama kuhusu hali ya utulivu nchini mwake baada ya shughuli za kijeshi za vikosi vya kimataifa vinavyoongozwa na jumuia ya kujihami ya NATO zitakapomalizika mwishoni mwa mwaka 2014 na pia uchaguzi wa rais nchini Afghanistan.
Mada zote hizo mbili zina umuhimu mkubwa kwa mustakbali wa nchi hiyo.Idadi ya wanajeshi watakaosalia ni muhimu kwa usalama na uchaguzi utabainisha njia gani itafuatwa na nchi hiyo inayozongwa na mizozo.
Mada nyengine zitahusiana na uchumi,uhusiano pamoja na nchi jirani na Afghanistan na hasa Pakistan na mazungumzo kuhusu uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya usalama kati ya Marekani na Afghanistan.
Wataalam wanakadiria vikosi vya Marekani na jumuia ya kujihami ya NATO vitakavyosalia Afghanistan baada ya mwaka 2014,vinaweza kufikia wanajeshi elfu 30. Hata hivyo raia wengi wa afghanistan wanahofia,maeneo ya kusini na mashariki ya nchi hiyo yanayopakana na Pakistan,yanaweza kuangukia mikononi mwa waasi,mara baada ya vikosi vya kimataifa vinavyoongozwa na NATO-ISAF vitakapoihama nchi hiyo.
Onyo kwa Pakistan
Ndio maana serikali ya Afghanistan inashikilia wanajeshi na polisi wapatiwe mafunzo na vifaa vya kimambo leo vya kijeshi.Msemaji wa rais Hamid Karzai Aimal Faizi amehakikisha mada hiyo itakuwa mojawapo ya mada muhimu katika mazungumzo kati ya rais Karsai na mwenyeji wake rais Barack Obama.
Ziara ya rais Hamid Karzai nchini Marekani imelengwa kutoa onyo kwa Pakistan na kwa wanamgambo wa Taliban.Dalili za kujongeleana zaidi Afghanistan na Marekani ni kishindo kwa Pakistan.Mtaalam wa masuala ya nchi za kusini mwa Asia Conrad Schetter anahisi hali hiyo itaifanya Pakistan ijaribu kuujongelea ushirika huo ili kuepuka isijikute ikitengwa.
Kwa kufanya ziara hii ya siku tatu nchini Marekani rais Hamid Karzai amewadhihirishia wataliban,serikali yake inajivunia uungaji mkono wa Marekani na kwamba mazungumzo ya amani hayataweza kufanyika kati yao na Marekani bila ya kuijumuisha serikali yake.
Mazungumzo ya amani pamoja na Taliban
Marekani,Afghanistan na Pakistan wanakubaliana kwamba mzozo wa Afghanistan hauwezi kufumbuliwa kwa mtutu wa bunduki.Wataalam wanahisi juhudi za kuendelezwa mazungumzo pamoja na wataliban walioko tayari kuzungumza,zinaweza kuleta tija pengine baada ya uchaguzi wa rais mwaka 2014.Marekani inaunga mkono mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Afghanisan na wataliban ili kuumaliza mzozo na pia kukamilisha shughuli za kijeshi za vikosi vyao.
Mwandishi:Hasrat-Nazimi,Waslat(DW-ASIEN)/Hamidou Oummilkheir
Mhariri:Yusuf Saumu